The House of Favourite Newspapers

Ukoo wa Kim Unaitawala Korea ya Kaskazini Tangu 1948

0

Mwandishi: Walusanga Ndaki | RISASI JUMAMOSI | Je Wajua?

JE, unafahamu kwamba Kiongozi wa sasa wa Korea ya Kaskazini, Kim Jong-un, ni mwendelezo wa utawala ulioanzia kwa babu yake wakati nchi hiyo ilipoingia katika ukomunisti?

Utawala huo ulianza Septemba 9, 1948 pale babu yake Kim Jong-un aliyeitwa Kim Il-sung alipoitangaza nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (JKWK) akiwa anaongoza Kamati ya Muda ya Umma ya Korea ya Kaskazini iliyokuwa imeanzishwa na Urusi baada ya Vita Kuu ya Pili.

Tangu hapo, viongozi wakuu wa nchi hiyo kupitia Chama cha Wafanyakazi cha Korea (CWK) kwa majina tofauti ya vyeo, wametoka katika familia au ukoo ulioanzia kwa Kim Ilsung.

Baada ya kifo cha Kim Il-sung, Julai 8, 1994, ambaye alitangazwa kuwa “Rais wa Maisha wa Jamhuri”, mwanaye, Kim Jong-il ndiye aliyeshika mikoba ya baba yake na kuongoza nchi hiyo.

Akiwa amejiimarisha madarakani, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CWK mwaka 1997, akachaguliwa Kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ulinzi ya Taifa mwaka 1988. Wakati wa utawala wake, alipewa nyadhifa kibao, hadi kifo chake Desemba 17, 2011.

Nafasi yake ilichukuliwa na mwanaye, Kim Jong-un, ambaye ndiye kiongozi wa sasa wa Korea ya Kaskazini tangu siku ya mazishi ya baba yake, Desemba 29, 2011.

Kwa kifupi, tangu mwaka 1948 utawala huo ulianzia kwa baba, ukaja kwa mwana na sasa unaendelea kwa mjukuu!

Ifahamike pia kwamba katika nchi hiyo kuna vyama vingine vya siasa viwili ambayo ni Korean Social Democratic Party na Chondoist Chongu Party. Hata hivyo, inasemekana vyama hivyo ni ushahidi tu wa mfumo wa vyama vingi nchini humo, kwani CWK ndiyo chenye madaraka siku zote na kwamba vyama vingine na viongozi wake ni nadra hata kutajwa.

Huo ndiyo ukoo wa Kim ambao umeshika uongozi nchini humo chini ya vyeo mbalimbali kupitia CWK kama vile Katibu Mkuu, Katibu wa Kwanza, Mwenyekiti, Rais na kadhalika.

Leave A Reply