The House of Favourite Newspapers

Ukweli Mpasuko Mastaa wa Injili

0

MAMBO ni mvurugiko kwa mastaa wa muziki wa Injili kutokana na viongozi wao kutifuana kisa vyama vinavyowasimamia, Risasi linakupa habari kamili.

 

Chanzo makini kililiambia gazeti hili kuwa ndani ya muziki wa Injili kwa sasa kuna mgogoro mzito kwa viongozi, hali ambayo inawaweka njia panda waimbaji kwa kuwa hivyo vyama ndivyo wanavyovitegemea kusimamia kazi zao na haki zao.

 

“Yaani ndani ya muziki wa Injili kwa sasa kuna fukuto la aina yake, viongozi wanagombana wenyewe kwa wenyewe kisa vyama na kujikuta wakiharibiana hata kwenye mambo ya msingi. Hali hii inawapa wakati mgumu sana waimbaji,” kilisema chanzo hicho.

 

Risasi Mchanganyiko lilianza na kumtafuta Katibu Mkuu wa Tanzania Music Foundation (TAMUFO), Stella Joel ili kueleza ukweli juu ya hilo ambapo alisema ni kweli upo mgogoro wa wao viongozi kuhusiana na vyama.

 

Aliendelea kusema kuwa Rais wa Chama cha Muziki wa Injili, Addo Novemba amekuwa akikizungumzia vibaya kuhusiana na chama chao cha TAMUFO, jambo ambalo linaumiza kwani wao kihalali yaani wanatambulika na serikali.

 

“Chama chetu sisi ni kwa ajili ya kuwasaidia wanamuziki wa Injili na wanamuziki wengine kwa ujumla ili waweze kufaidika na kazi zao, fursa mbalimbali pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali.

 

“Tumekuwa tukizunguka mikoa mbalimbali na kufanya mikutano ya fursa na kuunga mkono kazi zinazofanywa na serikali na wanamuziki kwa ujumla na mastaa wengi wameshanufaika na chama hiki zikiwemo fursa mbalimbali kama bima za afya na mengineyo.

 

Addo amekuwa akisema kwamba hiki siyo chama bali ni NGO, nimwambie tu yeye anasema kama nani, ni msajili wa vyama au vipi? Ukweli ni kwamba hiki ni chama kinachosaidia wanamuziki kwa ujumla na kuunga mkono juhudi za serikali na kila tunapokwenda Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) linajua, sasa sijui anataka nini zaidi.

 

“Kama kingekuwa chama cha utapeli, mastaa kama Bahati Bukuku, Upendo Nkone, Emmanuel Mbasha, Goodluck Gozbeth na wengine wengi wasingekuwepo, hivyo Addo asiongee vitu asivyokuwa na ushahidi navyo,” alisema Stella.

 

HUYU HAPA ADDO

Alipotafutwa Addo kwa ajili ya kuzungumzia hilo, alisema ukweli ni kwamba TAMUFO siyo chama, ni NGO ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Mzungu, aliposhindwa akarudi kwao na kuacha makaratasi, ndipo kina Stella wakaenda kuendeleza.

 

“TAMUFO siyo chama ni NGO, pia wanatapeli watu kwani kuna malalamiko kibao kutoka sehemu mbalimbali. Hivyo niwaambie tu mastaa wa Injili wawe makini.

 

“Tulienda kushughulikia mambo ya bima, tukaambiwa kwamba Stella kupitia TAMUFO alikwenda huko na kusema wao ndiyo wako hai lakini Chama cha Muziki wa Injili kilishakufa, ndipo wakapewa ushirikiano wao.

 

“Nasema Chama cha Muziki wa Injili hakijafa, bado kipo na tunaendelea na harakati za kukuza muziki wa injili zaidi na zaidi ila hii TAMUFO inatakiwa kuangaliwa kwa upya maana utapeli umejaa mno,” alisema Addo.

 

MBASHA NAYE ATOA NENO

Emmanuel Mbasha ambaye ni mmoja wa waimbaji wa Injili waliopo kwenye chama hicho cha TAMUFO ambaye alisema chama hicho kinawajali waimbaji kwa asilimia mia moja.

 

“Naipenda TAMUFO na nitaendelea kuipenda na sitaki kusikia unafiki wala mtu yeyote yule akiongea uongo juu ya viongozi wetu wakuu, hivyo nasema tupendane, tuhubiri injili daima,” alisema Mbasha.

STORI: Gladness Mallya, Risasi

Leave A Reply