The House of Favourite Newspapers

Ulinzi katika Hosteli za Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT Waimarishwa

0

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeimarisha ulinzi kwa kuongeza doria na vikundi vya Ulinzi Shirikishi katika Kata ya Luchelele Wilaya ya Nyamagana jijini humo.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa leo Desemba 20,2023 katika eneo la Mtaa wa Kisoko Kata ya Luchelele wakati wa kikao na Kiongozi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Wamiliki wa Hosteli, Vongozi wa Serikali za Mitaa na Wananchi wa Kata hiyo.

Akizungumza na Wananchi hao, Kamanda Mutafungwa amesema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Wamiliki wa Hosteli wanazoishi wanafunzi kwa kufunga CCTV Kamera kwenye nyumba zao na kuongeza ulinzi kwa kuajiri walinzi wa Kampuni Binafsi ili kuweza kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

“Ninawapongeza kwa kutuelewa pia ninawapongeza Askari waliofanya kazi kubwa ya kuimarisha ulinzi, lengo letu ni kukomesha vitendo vyote vya uhalifu”.. amesema Mutafungwa.

“Tunashukuru kuona mmeanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi, sisi tutawasaidia kuwapa mafunzo maana kutoa mafunzo kwa vikundi hivi ni kazi ya Jeshi la Polisi”…, ameongeza Kamanda Mutafungwa

Kwa upande wake, Padre Japhet Haule, Mlezi wa Wanafunzi katika Chuo cha SAUT amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kazi kubwa na nzuri ya kudhibiti uhalifu eneo hilo ambapo pia aliomba kuwekwa matuta katika Barabara zinazozunguka chuo hicho ili kudhibiti mwendo kasi wa bodaboda kwani wanahatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara.

Hata hivyo, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza , Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Sundy Ibrahim amewahakikishia Wananchi hao kumaliza kabisa kero ya usafiri eneo hilo na kwenda kukaa na watu wa TANROAD na kushauriana kuona namna ya kufanya ili kudhibiti mwendo kasi wa bodaboda eneo hilo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Mrakibu wa Polisi (SP) Virginia Sodoka amesema suala la ulinzi na usalama halina siasa hivyo ametoa onyo na kuwataka wamiliki wa hoteli ambao hawajaweka CCTV kamera waweke ili kuimarisha ulinzi.

Kuhusu wahalifu na watakaokamatwa kipindi hiki cha sikukuu, OCD Sodoka amesema watashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria. “Wahalifu wote watakaokamatwa kwa makosa mbalimbali katika kipindi hiki watatoka Kituo cha Polisi mwakani” amesisitiza Mrakibu Sodoka.

Leave A Reply