ULINZI SOKO KUU LA KARIAKOO, MLIMANCITY….RIPOTI MPYA!

kikosi kazi cha kufichua mauovu cha Global Publishers maarufu kwa jina la Oparesheni Fichua Maovu (OFM), kimeingia mzigoni kukagua usalama hususan Soko la Kariakoo na Mlimani City jijini Dar na kuibuka na ripoti mpya!

 

Awali, kwa nyakati tofauti OFM iliwahi kufanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko wa watu kama vile Mlimani City na Uwanja wa Taifa na kubaini udhaifu katika suala la ulinzi kwani, mtu ni rahisi kuingia na silaha yoyote bila kukaguliwa.

 

Katika uchunguzi mpya uliofanywa hivi karibuni na OFM, imebainika maeneo yenye ulinzi mzito ni katika Soko la Kariakoo jijini Dar na eneo la Mlimani City huku baadhi ya maeneo yakitahadharishwa kuongeza ulinzi ili kujiepusha na watu wenye nia mbaya kuweza kuingia kwa urahisi.

MPANGO KAZI WA OFM

Ili kujiridhisha na hali ya sasa, OFM walijipanga kwa kumuandaa ‘kamanda’ mmoja aliyekuwa amefunika sura akiwa ametinga baibui na kwenye mkoba wake akaweka vitu vya chuma vilivyoashiria kama silaha ili kuweza kujaribu kuingia navyo katika maeneo hayo yenye mikusanyiko ya watu. Baada ya ‘kujikoko’ kamanda huyo akiambataa na mwenzake, walifika katika jengo la Mlimani City na kukuta maeneo yote ya kuingilia kwenye maduka yakiwa na ulinzi wa kufa mtu tofauti na ilivyokuwa zamani.

 

Alipofika kwenye milango hiyo, alipekuliwa na kupitishiwa mashine maalum ya ukaguzi huku OFM mwingine akiwa makini kuchukua matukio hayo. Mbali na mashine hiyo maalum, walinzi hao walionekana kurandaranda sehemu mbalimbali za jengo hilo huku katika parking za magari, walinzi wakiwa juu kwenye vibanda vyao kuhakikisha wanalinda usalama.

Wanahabari wetu walizungumza na mmoja wa viongozi wa walinzi na kumuulizia jinsi walivyojipanga na matishio ya kigaidi kama yanayotokea nchi jirani kamanda huyo alisema wao wamejiimarisha vilivyo kama inavyoonekana na kuna ulinzi mwingine ni siri. “Huwezi kuona kila kitu kuna ulinzi mwingine tunawalinda bila nyinyi kujijua,” alisema mlinzi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

 

SOKO LA KARIAKOO

Baada ya kutoka kwenye jengo hilo lililokuwa na pilikapilika nyingi wanahabari wetu walienda Soko la Kariakoo ambapo nako ulinzi uliimarishwa kama Mlimani City. Wanahabari wetu walishuhudia magari yote yanayoingia shimoni kupeleka bidhaa yote yalikuwa yakikaguliwa kwa kifaa maalum mpaka uvunguni. Ukiachana na magari hata watu waliokuwa wakiingilia milango ya kupita watu nao walikuwa wakikaguliwa na vifaa maalum.

Baada ya kushuhudia zoezi hilo wanahabari wetu waliongea na askari waliokuwa wakilinda maeneo ya soko hilo ambapo walisema utaratibu huo una zaidi ya mwaka sasa lengo likiwa kuimarisha usalama na kuepusha madhara yanayotokea nchi nyingine.

 

Hata hivyo, OFM ilizungumza na mmoja wa watu waliokuwepo sokoni hapo ambaye alipongeza hatua hiyo lakini akatoa tahadhari katika majengo mengine ambayo yanakuwa na mkusanyiko wa watu.

 

“Hapa kwa kweli wanajitahidi kwa sasa lakini kipindi cha nyuma haikuwa hivi. Nafikiri ni wakati sasa kwa jeshi la polisi kuimarisha ulinzi sana hususan katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kwani kujilinda siku zote ni jambo jema kuliko kuamini tu kwamba tupo salama,” alisema jamaa huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Niki.

 

Niki aliongeza pia, kuna maeneo ya starehe ambayo bado suala la ulinzi ni changamoto kwani watu huingia bila kukaguliwa jambo ambalo ni hatari kwa watu wenye nia ovu.

Imeandikwa na Richard Bukos na Zaina Malogo.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma Leo Jan 31, 2019

Toa comment