The House of Favourite Newspapers

Tanzia: Mvumbuzi wa Tanzanite Afariki Dunia Muhimbili

TANZIA: Mvumbuzi wa Madini ya Tanzanite, Mzee Jumanne Ngoma amefariki leo Jumatano, Januari 30, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.

 

Mwaka jana, Mzee Ngoma alipatiwa msaada wa Tsh. Milioni 100 na Rais Dkt. John Magufuli kwa ajili ya kumsaidia katika matibabu yake ya ugonjwa wa kupooza uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Septemba 23, 1967, Bw. Ngoma alipewa barua na maabara ya Dodoma iliyosema madini hayo ni Zoisite. Hiyo ndio inajulikana hadi sasa kuwa ni tarehe rasmi ya ugunduzi wa Tanzanite duniani.

 

JUMANNE MHERO NGOMA-: MTANZANIA ALIYEGUNDUA MADINI YA TANZANITE AMEFARIKI DUNIA.

Bw. Ngoma alizaliwa mwaka 1939 kijiji cha Marwa, Same mkoani Kilimanjaro. Wazee wake walikuwa wakiishi Hedaru, walikuwa wafugaji na walikuwa wakihamahama kutafuta malisho. Mwaka 1952 walihama Hedaru na kuhamia Mererani.

Bw. Ngoma alisoma shule ya awali ya Town School, Arusha na kufaulu kuingia Mranda Middle school. Hata hivyo, hakuendelea na masomo baada ya baba yake kufariki na kukosa mtu wa kumlipia ada.

Siku moja, akiwa kijana mdogo, akiwa porini anachunga ngombe kwenye msitu uliopo Mererani ambao Wamasai huuita Lalouo, alifika eneo liitwalo Naisunyai ambalo lilitumiwa na wamasai kunyweshea ngombe maji.

Akaona vitu vinawaka na akapigwa butwaa akidhani ni nyoka wa aina ya kipekee. Akavisogelea akiwa na upinde na mshale tayari kwa lolote. Alipovigikia, akachukua mshale na kuanza kuvikwaruza vitu hivyo kimachale na kwa woga. Ghafla akaona vitu vya bluu vina’ngaa na akavipenda sana.

Ilimchukua muda mrefu akivishangaa vitu hivyo na ghafla akakumbuka alikuwa akichunga ngombe. Ikabidi awafuate ngombe alikowaacha lakini akakuta wametoroka. Ule ulikuwa msitu mkubwa na ilimchukua muda mrefu kuwapata na nyayo zao ndizo zilimsaidia kuwapata. Alipowapata ilikuwa tayari ni jioni sana hivyo akawarudisha nyumbani na kusahau kabisa mambo ya vile vitu vya bluu. Hakuvifuatilia tena.

Mwaka 1965, alimuoa Bi. Fatma Mauya. Mwaka 1966, Wizara ya madini litangaza mafunzo ya utafiti wa madini huko Morogoro. Bw. Ngoma akahudhuria na kuhitimu tarehe 6.6.1966.

Baada ya kupata mafunzo hayo, Bw. Ngoma alikumbuka vile vitu vya kun’gaa alivyoviona msitu wa Lalouo akiwa kijana, akahidi huenda yalikuwa ni madini. Akawaomba ndugu zake wamsindikize kwani ule ulikuwa msimu mnene.

Walipofika walichimba na kupata kilo 6 huku jiwe kubwa likiwa na uzito wa gram 55. Akayapeleka ofisi ya mkaguzi wa madini, Moshi kwa Bw. Bills. Mzungu huyo nguli, aliyatazama akasema hajawahi kuona madini ya aina hiyo toka azaliwe.

Ikabidi yapelekwe maabara ya serikali, Dodoma, lakini lile kubwa akabaki nalo. Kwa jinsi lilivyokuwa linang’aa, mke wa Bills alilipenda sana na akaliomba lakini Bw. Ngoma alimnyima.

Tarehe 23.9.1967, Bw. Ngoma alipewa barua na maabara ya Dodoma iliyosema madini hayo ni Zoisite. Hiyo ndio inajulikana hadi sasa kuwa ni tarehe rasmi ya ugunduzi wa Tanzanite duniani.

Pumzika salama Mzee Jumanne Mhero Ngoma.

Comments are closed.