The House of Favourite Newspapers

Ummy Mwalimu: Wakuu wa mikoa hakikisheni mnapambana na kipindupindu

0

1.Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto)akisoma taarifa yake na kulia kwake ni Naibu Waziri, Dk. Hamis Kigwangala anayesaidiana naye wizarani hapo, wakizungumza na wanahabari.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza wakuu wa mikoa, wilaya na kata kuhakikisha wanakuwa na kikosi kazi cha kupambana na kipindupindu na kutoa ripoti ya utekelezaji kwa ngazi za juu kila siku.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam akiwa makao makuu ya wizara yake, Mwalimu, amesema pamoja na kuwa na kuwa na vikosi vinavyoshughulikia masuala ya afya lakini, viongozi na watendaji wa mikoa na halmashauri wasimamie majukumu yao ya kukagua na kusimamia usafi katika kila kaya na kila siku ili kuboresha hali ya usafi na kuchukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka.
Mwalimu amesema shule zote pamoja na vyuo na taasisi zinazoendelea kutoa mafunzo zizingatie kanuni za afya ili kuzuia ugonjwa usiingie na kuenea katika maeneo yao.
Aidha aliwataja watu 11,257 waliopata ugonjwa huo tangu ugonjwa huo ulipoanza na kati yao jumla ya watu 177 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambao ni sawa na asilimia 1.5 ya waliougua.
Aidha, Waziri Mwalimu alitaja mikoa ambayo imekuwa na wagonjwa wengi tangu mlipuko uanze kuwa ni Dar es Salaam watu 4,628 ambayo ni asilimia 41 ya wagonjwa wote, ikifuatiwa na Tanga watu 1443 ambayo ni asilimia 13, Singida watu 955 ambayo ni asilimia 8, Mwanza watu 841 ambayo ni 7 asilimia.
Katika mazungumzo hayo, waziri huyo amepiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyomenywa na chakula katika maeneo ya wazi kutokana na kuibuka kwa kasi ya ugonjwa huo.
Pia amewaagiza maafisa afya kuhakikisha wauzaji wote wa vyakula wanazingatia kanuni za usafi ikiwa ni pamoja na kuosha vyombo kwa kutumia sabuni na kwa maji salama ya moto na sabuni.

NA DENIS MTIMA/GPL

 

Leave A Reply