‘OMOG afukuzwe’, ‘Omog abaki’, ‘Omog hatufai’, ‘Omog ni tatizo’, ‘timu hazichezi vizuri tatizo ni Omog’.
Hizo ni baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikitawala kwenye vyombo vya habari, mitandaoni, kwenye vijiwe na kwingine kote ambapo kuna mazungumzo kuhusu Klabu ya Simba.
Simba ipo katika nafasi ya nne ikiwa imezidiwa pointi mbili na Mtibwa Sugar ambayo inashika usukani katika Ligi Kuu Bara, pointi za Simba ni sawa na zile za wapinzani wao wa jadi, Yanga, wote wakiwa wameshinda michezo miwili na kupata sare mbili.
Ubingwa unawaniwa na timu zote lakini Simba kunaweza kuwa na presha kubwa zaidi ya timu nyingine zote kutokana na mazingira halisi ya timu hiyo hasa ni kutokana na kutumia kiwango kikubwa cha fedha katika usajili, pili ni kiu ya kuutaka ubingwa wa ligi hiyo baada ya Yanga kutawala kwa miaka kadhaa.
Omog amewahi kuipa ubingwa Azam FC, pia ndiye aliyeiwezesha Simba kupata nafasi ya kurejea katika michuano ya kimataifa, kwa wasifu wake katika soka la Afrika sina shaka na uwezo wake wa kufundisha hasa ukizingatia aina ya mazingira ambayo anafundishia.
Siyo lazima kocha bora afanikiwe katika kila timu anayofundisha lakini kuna wakati inategemea na mahitaji ya pande mbili, hapo namaanisha kocha anahitaji nini na kwa muda gani na pili ni uongozi nao unahitaji nini na kwa muda gani.
Katika kundi la pili wakati mwingine huwa linaongozwa na munkari wa mashabiki wao, mara nyingi mashabiki wanaweza kuwa na nguvu kubwa ya kushinikiza jambo fulani lifanyike na likafanyika kweli hata kama halikutakiwa kufanyika kwa wakati huo.
Omog ni kocha anayejielewa, amekabidhiwa timu ya msimu huu ikiwa ‘mpya’, nasema hivyo kutokana na aina ya usajili uliofanyika wakati msimu ukikaribia kuanza, ndiyo alipata muda wa kuwa na wachezaji kwa wiki kadhaa na hiyo ikamsaidia kuwajua na alitakiwa kupanga mipango yake kulingana na mahitaji ya timu na yaendane kwa wakati.
Usajili uliofanyika huku vyombo vya habari vikitumia nguvu kuwapamba wachezaji hao, kumewafanya mashabiki waamini Simba ina haki ya ushindi katika mechi zote, kinyume cha hapo kocha atakuwa hana msaada.
Nikukumbushe, Real Madrid iliwahi kuwa na kikosi cha mastaa wengi miaka kadhaa iliyopita, makocha wengi walishindwa kupata mafanikio makubwa kipindi hicho kutokana na presha na kukosa mtiririko sahihi wa kuwaunganisha mastaa hao.
Wiki kadhaa zilizopita niliandika makala katika kolamu hii nilieleza, Simba wanatakiwa kuwa makini katika kuwafanya mastaa wao kuwa wamoja, kuwa na wachezaji mastaa na kuwafanya wacheze kitimu ni vitu viwili tofauti.
Simba ya sasa inahitaji umoja na kumpa nafasi kocha afanye kile anachofanya ili akishindwa basi ahukumiwe kwa kile ambacho k i t a o n e k a n a uwanjani, takwimu hazidanganyi, soka ni mchezo wa takwimu pia.
Katika soka kuna kitu kinaitwa ‘chemistry’ yaani mu u n g a n i k o wa kuelewana baina ya mtu mmoja na mwingine, mfano Haruna Niyonzima akishika mpira anajua fulani ataelekea wapi au atafanya nini, hivyo chemistry kuna wakati huwa haipatikani kwa haraka.
Najua hizi kelele hazijatoka nje ya Simba tu, bali kwa asili ya soka letu lilivyo, kuna watu kutoka ndani ya Simba yenyewe ndiyo waanzilishi wa presha hiyo na wanachofanya ni kuseti mitambo tu ili ikikolea basi iwe rahisi kocha kufukuzwa.
Moja ya kitu ambacho Mungu ametujalia Watanzania ni kuwa wanafiki, huyo anayekuchekea usoni kumbe upande wa pili anakumaliza, ndani ya klabu zetu hizi kubwa huko hayo ndiyo maisha yao.
Hata kama Simba wenyewe wanakanusha nahisi mpishi wa kelele zote hizo ameanzia ndani ya nyumba yao. Tukumbuke kumfukuza Omog kisha kumleta kocha mpya hakutamaanisha ndani ya muda mfupi Simba itakuwa bingwa mapema.