The House of Favourite Newspapers

Unamsogeza karibu ya mumeo, usije kulia!

0

vegeterians-couple-bed

ASAALAM aleykum mashosti zangu popote pale mlipo. Najua kwa mwezi huu mtukufu, wengi wenu mtakuwa mmetulizana, ingawa zile harakati zetu za kishambenga hatuziachi, maana tuko katika swaumu, lakini bado tunasengenya, shoga kafanya hivi, ooh shosti kapora bwana wa mtu na nini sijui, Mungu hapendi mjue!

Wiki jana niliwajuza kuhusu wazugaji, sasa leo nina mada nyingine nataka kuzungumza na nyinyi, lakini kama ilivyokuwa wiki iliyopita, hii ninawaasa muache, vinginevyo mtaula wa chuya. Mashosti, enzi zetu mtu akiwa rafiki yako, basi mji mzima wanajua, Mwajabu na Mwajuma ni marafiki.

Si mmewahi kusikia kuhusu watu kuchanjiana hadi damu? Maana yake nini, kwamba sisi sasa ni ndugu, siri zako zote anazijua, ndugu zako wote anawajua na kila kitu chako. Urafiki huu ulizalisha undugu hadi watoto nao wakajua ni ndugu. Hata kwenye misiba, mtu angeweza kusubiri  kuzikwa hadi shogaye aje, ukiuliza imekuaje, unaambiwa hawa ni marafiki wa kuchanjiana.

Urafiki huu usingeweza kukutana na mambo yasiyofaa, mume wa Mwajabu angekimbia baa kama amekaa na mwanamke mwingine halafu amuone Mwajuma anakuja. Alijua habari lazima zimfikie mkewe na kama angemfuma, basi angeanza palepale kuomba radhi asimchongee kwa shoga yake.

Na mwanaume asingethubutu kumtongoza shoga wa mkewe, kwa sababu anajua kabisa kufanya hivyo ni sawa na kutangaza kuvunja ndoa yake. Sasa angalia mashosti wa siku hizi walivyo na marafiki zao. Siyo jambo la ajabu kuona mwanaume akiwa ametembea na marafiki wote wa mkewe na wala hawaoni tabu.

Ninataka kusema nini, mashosti msije kuwaamini rafiki zenu kuwaweka karibu na waume zenu. Utakuta rafiki yako anajitongozesha mwenyewe kwa mumeo na wanaume wenyewe walivyo wadhaifu, kufumba na kufumbua kitu na boksi!

Siyo kwamba rafiki yako asiwe karibu na mumeo, la hasha, lakini isiwe zaidi ya hapo. Utakuta shoga yako mazungumzo yakiwa ni juu ya mumeo, anachangia kila mada, anasifia na vitu kama hivyo, mmmh mwenzangu, jiongeze.

Zamani mwanaume wa mtu alikuwa mwangalifu sana wa kutongoza wanawake walio karibu na mkewe, hali siku hizi imebadilika kwa sababu na wadada wenyewe wamekuwa ‘maharage ya Mbeya’, utawasikia wakisema ‘shosti twende kwa mumeo akatupige ofa, tuna kiu!’

Kwa nini wao wasikuchukue uende kwa waume zao akakupe ofa. Kama unasoma na kusikia haya, au kama unasoma bila kuelewa, shauri yako ila kidonge changu kwa leo nd’o hicho, tukutane next week!

Leave A Reply