The House of Favourite Newspapers

Unategemea Akufurahishe Lakini Unaishia Kulia? Soma Hapa!

UHUSIANO wa kimapenzi una changamoto nyingi sana, idadi ya wanaolizwa na mapenzi inazidi kuongezeka kila kukicha, visa vya mapenzi vya kuumiza na kutoa machozi vinazidi kutokea kila kukicha kwa hiyo kuna umuhimu wa kutafuta elimu sahihi ya mapenzi kadiri iwezekanavyo.

Nimelazimika kuanza na maelezo hayo baada ya wiki iliyopita kukutana na kisa kinachomhusu msomaji wangu mmoja ambaye ameomba hifadhi ya jina lake. Tulianza kwa kuchati naye kwa meseji lakini alionesha kuwa na huzuni kali ndani ya moyo wake, maneno yake yalidhihirisha hilo.

Aliniambia kwamba yupo kwenye uhusiano na mwanaume anayempenda sana, ambaye walikubaliana waje kufunga ndoa na kuwa mume na mke halali, akajitahidi kadiri ya moyo wake wote kumpenda na kumtimizia mahitaji yake yote muhimu anayopaswa kutimiziwa na mkewe mtarajiwa.

Licha ya kujitoa kwa kadiri ya uwezo wake wote, dada huyu alinieleza kwamba, katika kipindi ambacho uhusiano wao ulikuwa umekaribia sana kuingia kwenye ndoa kama walivyokubaliana, alianza kuonesha mabadiliko ya waziwazi ya kitabia.

“Kwanza alianza kutopokea simu zangu kwa sababu tunaishi mbalimbali, hata nikimtumia meseji akawa hajibu kwa wakati, na hata akijibu anajibu kwa kifupi sana, tofauti sana na mwanzo wakati tunayaanza mapenzi yetu,” alisema dada huyo na kuendelea kueleza kwamba baada ya kuamua kumfuatilia kwa kina mwanaume huyo, alikuja kugundua kwamba kumbe alikuwa akitoka kimapenzi na msichana mwingine waliyekuwa wakiishi jirani, na siku nyingine walikuwa wakilala pamoja mpaka asubuhi.

Yote tisa, kumi ni kwamba dada huyo alienda mbele kwamba licha ya kugundua kwamba mwanaume huyo anamsaliti kwa kutoka kimapenzi na mtu mwingine, bado alipomuuliza akiwa na ushahidi alimjia juu kama mbogo na kutishia ‘kumfanyizia’ kama ataendelea kumfuatilia.

“Lakini nashindwa kumuacha kwa sababu nampenda sana na yeye ndiyo furaha yangu, siwezi kuishi bila yeye, naona kama dunia yote imefika mwisho,” alinieleza dada huyo siku nilipopata bahati ya kukutana naye ana kwa ana.

Nilichojifunza kupitia dada huyu, watu wengi hawajui thamani yao, wanawategemea watu wengine kuwapa furaha ya kudumu maishani na inapotokea mambo yameenda ndivyo sivyo, wengine wanafikia hata hatua ya kuyakatisha maisha yao kwa sababu wanaamini hawawezi kufurahi tena, hawawezi kusimama tena maishani mwao, hawawezi kufanya chochote kwa sababu wale waliowapenda na kuwapa nafasi ya kuitawala mioyo yao, wamewaumiza na kuwasababishia msiba kwenye mioyo yao.

Sitaki kumbeza mtu anayeumiza kwa sababu ya mapenzi, maumivu ni hisia kama hisia nyingine, utakuwa unajidanganya pale unapoumia halafu ukawa unajifanyisha kwamba hujaumia. Kuukataa ukweli ni tatizo, lazima ukubaliane na ukweli kwamba suala la kuumizana kwenye mapenzi lipo na halikwepeki, yawezekana leo una furaha lakini ipo siku atakuumiza moyo wako mpaka utatamani ardhi ipasuke uingie!

Maumivu yapo na hayakwepeki lakini jambo la msingi unalopaswa kulijua ni kwamba, ni makosa makubwa kutegemea mtu mwingine ndiyo awe furaha ya kudumu kwenye maisha yako.

Ukweli ambao watu wengi hawaujui, ni kwamba wewe ndiyo unayepaswa kuwa chanzo cha furaha yako, wengine wawe wa ziada tu, usimpende mtu mpaka ukasahau kujipenda wewe mwenyewe. Ukiweza kujipenda wewe mwenyewe kwanza, kisha ndiyo akafuata mumeo, mkeo, mchumba wako au mpenzi wako, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuhimili changamoto za kimapenzi, hata kama zitakuwa kubwa kiasi gani.

Wiki ijayo nitakueleza namna ya kuanza kujipenda wewe mwenyewe kwanza, ili hata ikitokea mtu ameuumiza moyo wako uweze kusonga mbele bila kutetereka sana.

Tukutane wiki ijayo.

Comments are closed.