The House of Favourite Newspapers

Unategemea Akufurahishe, Unaishia Kulia? Soma Hapa-2

0

NI wiki nyingine ninapokukaribisha jamvini msomaji wangu, mada ya leo ni ile tuliyoanza nayo wiki iliyopita, ambapo nilikueleza kwamba kama unaishi kwa kutegemea furaha yako itatoka kwa mpenzi wako, basi unafanya makosa makubwa kwa sababu hutaipata hiyo furaha na matokeo yake, utakuwa mtu wa kulia kila siku.

 

Sikatai kwamba wapo watu ambao katika mahusiano, huwa waaminifu sana, wenye huruma na wenye mapenzi ya dhati, ambao ukiwa nao utajihisi kuwa na amani ya kweli ndani ya moyo wako, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba akili ya binadamu inaweza kubadilika wakati wowote na akawa tofauti kabisa na vile ulivyomzoea.

 

Jambo la muhimu, unatakiwa kujenga misingi imara kuanzia ndani yako mwenyewe, kama ni mapenzi ya dhati, basi unatakiwa kujipenda wewe mwenyewe kwanza. Yawezekana unampenda sana na upo tayari kufanya chochote kwa ajili yake, lakini je, unaitambua thamani yako? Huwezi kuitambua thamani yako mpaka pale utakapoanza kujipenda. Lazima ujiulize, wewe ni nani, ilikuwaje ukaja hapa duniani na nini hasa kilichokuleta hapa duniani.

 

Kumbuka ulikotoka, lielewe chimbuko lako, ielewe historia yako na jikumbushe malengo uliyojiwekea. Tambua kwamba ili malengo yako yatimie, lazima uwe na afya nzuri ya mwili na akili na migogoro ya kimapenzi ni miongoni mwa mambo yanayoweza kukurudisha nyuma kama utaipa nafasi kubwa kwenye maisha yako.

 

Ukifikia hatua hiyo, tayari utakuwa umeanza kutambua thamani ya maisha yako na kubwa kuliko yote, lazima utambue kwamba mapenzi siyo kila kitu kwenye maisha yako bali ni sehemu ya maisha yako. Hakuna mtu amewahi kufa kwa kukosa mpenzi, la hasha lakini wapo
wengi waliokufa kwa kupata wapenzi wasio sahihi. Pata muda wa kutosha wa kupumzika ukiwa peke yako na hii inatakiwa kuwa kila siku. Hakikisha unakula vizuri, unapata muda wa kulala na unatimiza majukumu yako ya kila siku kikamilifu. Kama ni mfanyakazi, hakikisha unafanya kazi kwa umakini, kama ni mfanyabiashara hakikisha pia kwamba unasimamia vizuri shughuli zako za kila siku.

 

Pale unapopata muda au nafasi, jipongeze mwenyewe. Tenga muda wa kuwa unatoka kwenda maeneo kama ufukweni au sehemu nyingine tulivu ukiwa peke yako. Inaweza kuonekana kama jambo la ajabu kwa sababu wengi wamezoea kwamba wakitoka, lazima waambatane na wapenzi wao. Unatoka naye ‘out’ kwa sababu unampenda lakini unapotoka mwenyewe, maana yake unajipenda wewe zaidi. Epuka tabia hatarishi kama vile ulevi na tabia ya kuwa na uhusiano na zaidi ya mtu mmoja kwa wakati mmoja kwani hayo ni miongoni mwa mambo yatakayokufanya usitimize ndoto zako.

 

Kwa imani yako, pata muda wa kuwasiliana na Mungu wako, pale unapokutana na mambo magumu, mshirikishe yeye na muombe akuongoze katika njia iliyonyooka. Utashangaa sana kwamba ukizingatia haya yote, moyo wako utakuwa na amani ya kutosha, utajisikia furaha kutoka ndani ya moyo wako na wala hutamtegemea tena mtu mwingine akufurahishe. Ukiwa na hali hii ya utulivu kutokea ndani, itakuwa rahisi kwako kuishi na mpenzi wa aina yoyote kwa sababu furaha yako haitamtegemea mtu, itakuwa inatoka ndani yako mwenyewe kwa hiyo hata pale utakapoona mambo hayaendi kama ulivyotegemea, utakuwa mwepesi wa kuchukua hatua bora zaidi. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi.

Hashim Aziz +255 719401968

Leave A Reply