The House of Favourite Newspapers

Unaumia Kusikia Uliyenaye Ameshatembea na Wengi? Soma Hapa

0

55534.jpg

KWA neema yake Mungu, ni Jumamosi nyingine tunapokutana mimi na wewe kupitia ukurasa huu. Hapa marafiki zangu tunajadili na kujifunza kwa pamoja kuhusu elimu ya uhusiano. Ukiweka dhamira ya kujifunza naamini hutatoka hivihivi.
Kuna kasumba moja imejengeka katika mioyo ya watu, kwamba kitu kinakuwa na thamani kinapokuwa chako. Kikihamishwa umiliki na kwenda kwa mwingine, mmiliki wa awali hana cha kuzungumza zaidi ya kukikosoa.

Kitu hicho kitaonekana hakina thamani. Kitazuliwa kila lililo baya. Mmiliki wa awali atajitahidi kufanya kila aina ya mbinu anayoijua kuhakikisha jamii nzima inafahamu kwamba kile kitu si chochote, si lolote. Anakuwa hodari kweli wa kukielezea kitu hicho akiamini ni sifa kwake.

Hapo nina maana gani? Kuna baadhi ya wanaume wapo hivyo. Mtu akitembea na mwanamke fulani, ikitokea wameachana, anatumia nguvu nyingi kueleza ubaya au uzuri wa mwenzake.
Kwenye ubaya anamponda, kwenye uzuri anakejeli kwa kauli zile za ‘nishamfaidi yule hawezi kuniringia, kwanza atanieleza nini?’.

Japo tatizo hilo linaweza kufanywa pia na wanawake lakini inaaminika zaidi wanaume ndiyo wanaongoza kwa kusambaza au kuponda kuhusu wanawake walioachana nao. Wanakwenda mbali zaidi kwa kusambaza habari hizo kiasi ambacho kinageuka maumivu kwa yule mchumba mpya wa huyo mwanamke.
Kitu cha kujifunza hapa ni nini? Kujitambua. Unapoingia kwenye uhusiano halafu ukisikia mtu wako alikuwa na mtu mwingine, usishtuke! Jiulize unataka kuelekea wapi? Kama kweli una mpango wa kufika mbali na huyo mtu hupaswi kukatishwa tamaa na taarifa hizo.

Chukulia ni jambo la kawaida. Huna sababu ya kukasirishwa na taarifa za kuwa mtu wako alishatembea na fulani kwani katika ulimwengu wa leo, kila utakayekutana naye lazima alikuwa na mtu. Yawezekana kabla yako kuna wengine watano au sita wamekutangulia, hilo lisikukatishe tamaa.
Chukulia kwamba ndiyo uhalisia wa maisha. Ni nadra sana kumkuta mtu akiwa hajatanguliwa na wenzako. Suala la msingi ni kujua dira yenu katika safari yenu ya uhusiano. Kujua msimamo wa huyo mwenzako. Mkilitambua  hilo, hakuna kitakachowashinda.

Kelele za watakaosema wametembea na mtu wako zitafanana na zile za chura, haziwezi kumzuia tembo kunywa maji. Zichukulie kama changamoto. Kikubwa cha kuzingatia ni msimamo. Kwa pamoja mnapaswa kuwa na msimamo kuhusu kile mnachokisimamia.

Mwanamke kutoka moyoni anapaswa kusahau alikotoka. Aangalie mbele. Aoneshe kweli kutoka moyoni kwamba amedhamiria kusafiri. Asitiliwe shaka hata chembe na mwenzake juu ya kule alikotoka.
Awe balozi mzuri wa penzi jipya. Aweze kulitetea mahali popote. Awe na uthubutu wa kutamka moyoni na mdomoni kwamba huyu ndiye wangu. Huko kote alikopita ilikuwa ni mazoezi na sasa ameingia kwenye mechi. Amefika Kigoma mwisho wa reli.

Ajue kwamba ni msimamo na uaminifu pekee ndiyo unaoweza kumtoa mashaka mwenzake. Ajue kabisa hakuna mwanaume kama huyo aliyenaye. Akizingatia hayo, hakuna kitakachomrudisha nyuma. Hakuna changamoto itakayokuwa nje ya uwezo wake.

Atakuwa ameshampa ujasiri mwenzake. Naye atapambana kutetea pendo lake. Hata wakusanyike watu wanaoweza kujaza uwanja wa taifa waseme kwamba walishatembea naye, bado atajiona yeye ndiye mwenye bahati kwa kuwa naye wakati huo na kufanya maisha.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kuvutia!

Leave A Reply