The House of Favourite Newspapers

UNDANI SIKU 8 ZA SOUDY BROWN, MAUA SAMA LUPANGO

 LICHA ya kuachiwa kwa dhamana, Mtangazaji maarufu wa Kipindi cha Shilawadu, Soud Brown na msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama wamehenyeshwa kwa takriban siku 8 lupango, Risasi Mchanganyiko linakupa undani wa sakata hilo.  

 

Soud na Maua walikamatwa na polisi Septemba 16, mwaka huu wakidaiwa kudhalilisha nembo ya taifa kwa kuchezea fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati wakiwa mahabusu, Soud alipata msala mwingine wa kudaiwa kutumia maudhui ya mtandao bila kuwa na kibali. Msala unaowagusa wote wawili ni ule wa kurusha kipande cha video kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii kinachoonesha watu wasiofahamika majina yao, wakicheza wimbo wa Maua uitwao Iokote huku wakitupa hela juu na kuzikanyaga.

 

Awali, wawili hao walitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni kisha baadaye wakapelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, wakawekwa ndani wakati jeshi hilo lilipoanza uchunguzi wake. Hata hivyo jeshi hilo liliendelea na uchunguzi wake kwa takriban siku 7 na ilipofika siku ya 8 (Septemba 24, mwaka huu), Soud pekee ndiye aliyepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu.

 

Tofauti na shtaka lililofahamika awali, Soud alipandishwa peke yake mahakamani hapo sambamba na washtakiwa wengine kwa kosa la kutumia maudhui ya mtandao. Wakili wa Mkuu Serikali, Faraja Nguka akishirikiana na Wakili Estazia Wilson walimsomea shtaka hilo Soud Brown mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustino Rwizile.

Nguka amedai kati ya Juni 11 na Septemba, 2018 Dar es Salaam kwa kutumia online TV inayojulikana kwa jina la Shilawadu TV, kinyume cha sheria alitoa maudhui katika mtandao huo bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

 

Hata hivyo wakili Peter Kibatala anayemtetea Soud aliomba mteja wake huyo apewe dhamana kwa sababu shtaka linadhaminika. Hakimu Rwizile akitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo, alimtaka awe na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya shilingi milioni 2, pia mshtakiwa mwenyewe asaini bondi ya shilingi milioni 2.

 

Soud alifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 18, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la. Hata hivyo, mara baada ya kusomewa shtaka hilo na kupata dhamana, Soud alikamatwa tena na kurudishwa katika kituo Kikuu cha Polisi kuendelea kushikiliwa kwa ajili ya kesi yake ya awali ya kudhalilisha nembo ya taifa. Uchunguzi wa kesi hiyo utakapokamilika, Soud na Maua wanatarajiwa kupandishwa kizimbani.

 

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.