The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 58

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inaanza. Upande wa pili, Suleikha anazidi kumganda Jafet kama ruba na sasa wapo pamoja chumbani. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Walienda moja kwa moja mpaka hosteli, wakapitiliza mpaka kwenye chumba alichokuwa anaishi Suleikha, akamkalisha Jafet juu ya kitanda kisha akaenda kufunga mlango kwa funguo, Jafet akawa ametulia kama kondoo anayesubiri kuchinjwa.

“Unajua kwa nini nimekuleta huku?” alisema Suleikha huku akimsogelea Jafet pale alipokuwa amekaa kwa mwendo wa maringo utafikiri mwanamitindo wa kimataifa, Naomi Campell. Jafet hakujibu kitu zaidi ya kutingisha kichwa huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Suleikha akamvamia mwilini na kumkumbatia kimahaba, kufumba na kufumbua wakagusanisha ndimi zao mithili ya njiwa anayemlisha kinda wake. Kwa mara ya kwanza Jafet naye akawa anatoa ushirikiano kwa msichana huyo mrembo, ukichanganya na mvinyo uliokuwa umekolea kwenye vichwa vyao, hakuna aliyemuonea mwenzake aibu.

“Laki…ni Sulei…kha!”
“Lakini nini Jafet!”
“Niliweka nadhiri kwamba sitafanya chochote na mwanamke yeyote mpaka nitakapofunga ndoa.”

“Hata mimi niliweka nadhiri ya kutompa mwanaume yeyote mwili wangu mpaka nitakapoolewa lakini nimeamua kukutunuku wewe,” alisema Suleikha kwa sauti ya chini iliyokuwa inatoka kupitia matundu ya pua zake.

Wawili hao waliendelea kupasha miili yao moto tayari kwa pambano hilo lisilo na refa wala jezi na hatimaye wakajikuta wakiangukia dhambini.
“Suleikha!”
“Abee.”

“Sitaki kuamini kwamba kweli ulikuwa humjui mwanaume, ahsante sana kwa zawadi nzuri uliyonipa, hata siamini,” Jafet alisema lakini badala ya kumjibu, Suleikha aligeukia upande mwingine huku akionesha kuugulia maumivu makali.

Isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuamini kwamba msichana huyo, licha ya urembo wa kipekee aliokuwa nao, hakuwa akimjua mwanaume yeyote.
Lile wingu la huzuni lililokuwa limeuzingira moyo wa Jafet kwa kipindi kirefu baada ya kuachwa na Anna, liliyeyuka kama barafu iyeyukavyo juani.

“Nisamehe kwa kushindwa kukuonesha mapenzi kama unayonionesha wewe kwa kipindi chote hiki, nilikuwa nimechanganyikiwa kutokana na nilichofanyiwa na Anna lakini leo ndiyo nimeamini kwamba unanipenda kwa dhati na naahidi kukupenda pia,” Jafet alizungumza kwa sauti ya kubembeleza lakini Suleikha hakumjibu chochote.
Akaendelea kumbembeleza na kumsihi aamini kwamba na yeye anampenda kwa moyo wake wote.

“Unaniahidi nini Jafet?”
“Naahidi kuwa nitakupenda na kukutunza kwa kadiri ya uwezo wangu wote.”
“Utanioa?”

“Lazima nikuoe Suleikha,” alisema Jafet huku akionesha kumaanisha kile alichokisema, kauli iliyomfanya Suleikha amkumbatie kwa nguvu.
“Naomba usinidanganye Jafet, niko chini ya miguu yako.”

“Siwezi kukudanganya mpenzi wangu, nimeamini unanipenda kwa dhati kwa sababu kama isingekuwa hivyo tayari ungeshachoka na kuniacha,” alisema Jafet na kumbusu Anna kwenye paji la uso wake. Waliendelea kupiga stori za hapa na pale, baadaye Suleikha akamsindikiza Jafet mpaka kwenye hosteli aliyokuwa anaishi. Huo ukawa mwanzo wa kufungua ukurasa mpya wa mapenzi kwa Jafet na Suleikha.

Wikiendi wawili hao walitoka pamoja na kwenda ufukweni ambapo walioneshana mapenzi mazito kiasi cha kila aliyekuwa anawaona kuwaonea wivu. Wakawa wanacheza kwenye mchanga wa bahari, kunyweshana juisi na kucheza kila aina ya mchezo wa kufurahisha.
***
Maandalizi yaliendelea kufanyika na baada ya kila kitu kukamilika, Anna aliingizwa kwenye chumba maalum ambapo kazi ya kumtoa ujauzito wake ilianza chini ya usimamizi wa madaktari wazoefu. Kwa kuwa ujauzito huo ulikuwa mdogo, haikuwa kazi kubwa kwa madaktari hao.

Hatimaye zoezi hilo likakamilika ambapo ilibidi Anna apumzishwe wodini kwa saa kadhaa.

Saa kumi na mbili jioni, Anna alichukuliwa na wazazi wake na kurudishwa nyumbani huku bado akiwa anaugulia maumivu makali. Akawa anaendelea kutumia dawa alizopewa hospitalini. Siku hiyo ilipita, wazazi wake wakawa wanaendelea kumpa moyo kwani tayari daktari wake alishawaambia kwamba anahitaji kutulizwa kisaikolojia.

Wiki moja baadaye, tayari alikuwa na ahueni kubwa lakini kama ilivyokuwa siku za nyuma, alianza kulalamikia maumivu makali kifuani, upande ule aliopandikizwa figo
Hali hiyo iliwapa hofu kubwa wazazi wake, wakalazimika kumrudisha hospitalini haraka iwezekanavyo ambapo alipofikishwa tu, alianza kuchukuliwa vipimo.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply