The House of Favourite Newspapers

Unending love – 59

0

(PENZI LISILOISHA)-62
Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa.

Upande wa pili, Suleikha anazidi kumganda Jafet kama ruba na kwa mara ya kwanza, wawili hao wanakutana kimwili, kila mmoja ikiwa ndiyo mara yake ya kwanza kuingia kwenye ulimwengu huo wa kikubwa. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Wikiendi, Suleikha na Jafet walitoka pamoja na kwenda ufukweni ambapo walioneshana mapenzi mazito kiasi cha kila aliyekuwa anawaona kuwaonea wivu. Wakawa wanacheza kwenye mchanga wa bahari, kunyweshana juisi na kucheza kila aina ya mchezo wa kufurahisha.

Penzi jipya kati ya Jafet na Suleikha lilizidi kupamba moto hasa baada ya wawili hao kuvunja mwiko ambao kila mmoja alikuwa amejiwekea wa kutokutana kimwili kabla ya ndoa.

“Unajua kuna kipindi nilikuwa naamini kama siwezi kuja kupenda tena, nimepitia kipindi kigumu sana maishani mwangu kwa sababu ya mapenzi, Anna aliniumiza sana moyo wangu.”

“Pole kipenzi changu, nipo kwa ajili ya kuutibu moyo wako na nakuhakikishia nitafanya kila kitu ili kuiponya nafsi yako,” alisema Suleikha na kumbusu Jafet kimahaba.

Ndani ya kipindi kifupi tu tangu walipohalalisha rasmi uhusiano wao wa kimapenzi, Jafet alikuwa na mabadiliko makubwa sana, kuanzia kimwili mpaka kiakili. Mwili wake ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa umepungua sana kwa sababu ya mawazo, ulianza kunawiri na kumfanya awe na mwonekano wa kuvutia.

Hata uelewa wake darasani uliongezeka maradufu, akawa anaweza kufanya majadiliano ya vikundi (group discussion) na wanachuo wenzake, jambo ambalo kwa kipindi kirefu alikuwa akishindwa kulifanya kutokana na kupenda kujitenga, akimuwaza sana Anna.
“Mshkaji kumbe huwa unaweza kutabasamu?”

“Swali gani hilo? Kwani kuna mtu huwa hawezi kutabasamu?”
“Kwako ilikuwa tofauti kwa sababu tangu nikujue hapa chuoni sijawahi kukuona ukitabasamu, muda wote ulikuwa mtu wa kujiinamia tu lakini sasa hivi nakuona tabasamu pana muda wote, nini siri ya mafanikio yako?” Lazaro, mwanachuo aliyekuwa akisoma pamoja na Jafet alimtania rafiki yake huyo, Jafet akaishia kucheka tu kwani kilichosemwa kilikuwa sahihi.
“Napenda kukuona ukiwa na furaha kiasi hiki, nataka dunia nzima ijue kwamba nakupenda,” alisema Suleikha kwa sauti ya chini baada ya kumsikia Lazaro akimtania Jafet.
“Ahsante Suleikha, wewe ni mwanamke wa tofauti sana, nakupenda sana,” alisema Jafet kwa sauti ya kunong’ona, majadiliano ya kimasomo yakaendelea.
Siku zilizidi kusonga mbele, Jafet akawa anazidi kubadilika kwani ukiachilia mbali mapenzi ya dhati aliyokuwa akipewa na Suleikha, msichana huyo pia alikuwa akimpa misaada mbalimbali ya kifedha kwani naye alikuwa akitokea kwenye familia inayojiweza kiuchumi.
“Hatujawahi kuzungumzia kuhusu familia yako Suleikha.”
“Mh! Sidhani kama ni muhimu sana kuhusu hilo.”
“Hapana, mimi na wewe siku baadaye tutakuwa mume na mke, ni vizuri tukawekana wazi kwa kila kitu, au we unaonaje?”
“Mimi baba yangu ni mfanyabiashara. Unajua asili yetu sisi ni Uarabuni na ndiyo maana unaniona hata mimi niko na mchanganyiko. Baba asili yake ni Dubai, Falme za Kiarabu lakini mama ndiyo Mtanzania, Msambaa wa Magoma, Korogwe mkoani Tanga.”
“Ok, nimefurahi kufahamu hilo. Kwa hiyo baba yako anashughulika na biashara gani?”
“Ni mfanyabiashara wa magari, huwa anaagiza kutoka nje na kuja kuyauza kwenye showrooms (maduka ya magari) zake za hapa Dar es Salaam,” alisema Suleikha lakini tofauti na alivyotegemea, maelezo hayo yalikuwa sawa na mkuki ndani ya moyo wake.
Kwa maelezo hayo mafupi aliyoyatoa, Jafet alielewa msichana huyo anatoka kwenye familia yenye uwezo mkubwa kifedha, pengine kuliko hata familia ya Anna na tayari ndani ya kichwa chake, alishajiapiza kwamba hataki tena msichana kutoka familia ya kitajiri.
Maneno ya mama yake aliyowahi kumwambia wakati akiteswa na Anna kwamba hakuwa na hadhi ya kuoa tajiri kwa sababu yeye alitokea familia maskini, yalikuwa yameshaota mizizi ndani ya kichwa chake.
“Vipi mbona umeonekana kuwa mnyonge baada ya kukujibu hivyo?”
“Kwa nini hukuniambia kutoka mwanzo Suleikha?”
“Kukwambia nini Jafet?”
“Kwamba unatokea familia ya kitajiri? Mbona nilishakueleza kutoka mwanzo kwamba natokea katika familia maskini na nataka mwanamke anayetokea kwenye familia maskini pia?”
“Sikukwambia ukweli kwa sababu mimi nimekupenda kwa moyo wangu wote kwa sababu ya umaskini wako.”
“Wewe inawezekana umenipenda vipi kuhusu wazazi wako?”
“Baba yangu ni ‘mzungu wa roho’ sana! Hawezi kuleta uswahili wa kiasi hicho, kwetu sisi binadamu wote ni sawa, amini ninachokwambia,” alisema Suleikha na kuendelea kumsisitiza Jafet kutokuwa na wasiwasi wowote kuhusu suala hilo.
“Na nakuhakikishia, kwa mfano ikitokea wazazi wangu wakataka kuleta kipingamizi chochote, nipo tayari kuyakatisha maisha yangu lakini siyo kuishi mbali na wewe Jafet. Wewe ndiyo mwanaume wa kwanza na wa mwisho katika maisha yangu, amini ninachokwambia,” alisema Suleikha huku akilengwalengwa na machozi.
Maneno hayo yakaonekana kumuingia Jafet ambaye alishusha pumzi ndefu na kumsogelea Suleikha.
“Unaniahidi utakuwa na mimi licha ya umaskini wa familia yetu?”
“Nakuahidi mume wangu mtarajiwa.”
“Ahsante kwa kunipenda Suleikha, na mimi naahidi nitakuwa na wewe kadiri ya uwezo wangu wote,” alisema Jafet na kumkumbatia Suleikha kimahaba. Muda mfupi baadaye, wawili hao waligusanisha ndimi zao na kuanza kuwaiga njiwa wanavyoyalisha makinda yao.
***
Wiki moja baadaye, Anna tayari alikuwa na ahueni kubwa na zoezi la kumtoa ujauzito kihalali likawa limekamilika lakini kama ilivyokuwa siku za nyuma, alianza kulalamikia maumivu makali kifuani, upande ule aliopandikizwa figo.
Hali hiyo iliwapa hofu kubwa wazazi wake, wakalazimika kumrudisha hospitalini haraka iwezekanavyo ambapo alipofikishwa tu, alianza kuchukuliwa vipimo.
“Mungu wangu, inaonekana kuna tatizo kwenye figo aliyopandikizwa, imeharibika kutokana na kushindwa kufuata dozi ya dawa alizoandikiwa na pia kwa sababu ya matumizi ya pombe, inabidi alazwe haraka sana,” alisema daktari aliyempokea Anna katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
Wazazi wake hawakuwa na cha kufanya, mipango ikafanyika haraka ambapo Anna alilazwa kwenye wodi maalum na kutundikiwa dripu huku madaktari wakiitana kwa dharura kujadiliana juu ya namna ya kumsaidia msichana huyo.

Leave A Reply