The House of Favourite Newspapers

Unending love -65

2

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa lakini matatizo mengine ya figo yanazuka upya na kusababisha asafirishwe mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet atafutwe mahali popote alipo na kupelekwa hospitalini hapo. Kazi hiyo inafanyika na hatimaye Jafet anaenda kuonana na Anna hospitali.

Baba yake Anna anambembeleza kijana huyo ajifanye amemsamehe Anna na kurudiana naye ili kumfariji kwenye kipindi kigumu alichokuwa anapitia, jambo linaloonekana kumkwaza sana Suleikha.

Kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya, madaktari wanashauri arudishwe nchini India na bila kupoteza muda, mipango ya safari inaandaliwa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Siku tatu baadaye, Anna na wazazi wake wote wawili, walikuwa ndani ya ndege kwa safari ya kuelekea nchini India kwa matibabu zaidi ya binti yao ambaye kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo afya yake ilivyokuwa inazidi kudhoofika.

Baada ya kusafiri kwa saa nyingi angani, hatimaye ndege kubwa, mali ya Shirika la Fly Emirates iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Chhatrapati Shivaji jijini Mumbai, India. Wakateremka na kukamilisha taratibu zote uwanjani hapo na kutoka kwenye geti kubwa (terminal one) ambako waliwakuta wahudumu wa Hospitali ya Apollo wakiwa wanawasubiri na gari maalum la kubebea wagonjwa.

Muda mfupi baadaye, Anna tayari alikuwa ndani ya ‘ambulance’, akiwa amezungukwa na manesi wachangamfu wa Hospitali ya Apollo. Wazazi wake walikuwa wamepanda kwenye gari jingine na safari ya kuelekea hospitalini ikaanza.

Baada ya kufikishwa hospitalini hapo, Anna alipandishwa kwenye kitanda maalum cha magurudumu na kupelekwa wodini ambako alianza kuandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye vipimo.

Kama ilivyokuwa kawaida ya hospitali hiyo, Anna alipopelekwa maabara, alianza kufanyiwa vipimo vya kila kitu, kuanzia wingi wa damu, kundi la damu, mapigo ya moyo, wingi wa sukari katika damu na vipimo vingine kedekede.

“When your daughter was transplanted a kidney here, we gave you all the necessary procedures and precautions she needs to take in order to prevent organ rejection. Why did’nt you make her adhere to them?”

(Binti yenu alipokuja kupandikizwa figo hapa, tulimpa masharti na maelekezo ya nini cha kufanya ili kuzuia mwili wake usiikatae figo aliyopandikizwa. Kwa nini hamkumfanya afuate maelekezo hayo?)

“We are sorry doctor, she has been studying in America for so long, that’s why we failed to take care of her,” (Tusameheane daktari, kwa kipindi kirefu alikuwa anasoma nchini Marekani ndiyo maana tulishindwa kumsimamia) baba yake Anna alijitetea baada ya Dokta Shivji ambaye ndiye aliyesimamia matibabu yake awali, kuanza kuwabana kwa maswali.

Majibu hayo ya baba yake Anna, yalimsikitisha mno daktari huyo kwani kwa jinsi kazi ya kumpandikiza figo mpya msichana huyo ilivyokuwa ngumu, hawakudhani kwamba itaharibika kizembe namna hiyo ndani ya kipindi kifupi.

Baada ya maelezo hayo, Dokta Shivji alitoka na faili lenye majibu ya msichana huyo na kwenda nalo kwenye ofisi ya madaktari wenzake ambapo walianza kujadiliana nini cha kufanya.

Kila mmoja alionesha kusikitishwa na uzembe uliosababisha figo aliyopandikizwa Anna kuharibika haraka kiasi hicho. Kilichozidi kuwachanganya akili, kulikuwa na watu wachache sana ambao figo zao zilikuwa zikiendana na za Anna hivyo suala la kumpata mtu mwingine kwa ajili ya kumtolea tena figo Anna halikuwa jepesi.

“But there is an alternative doctor, while we awaits another donor, we may start to administer her with dialysis,” (Lakini kuna njia mbadala daktari, wakati tunasubiri mtu mwingine wa kujitolea figo, tunaweza kumuanzishia matibabu ya kumsafisha damu kwa mashine maalum) alisema daktari mwingine wakati mjadala wa namna ya kumsaidia Anna ukiendelea, wazo lililoonekana kuungwa mkono na karibu watu wote.

Baada ya kukubaliana, ilibidi Dokta Shivji awaite wazazi wa Anna ofisini kwake na kuanza kuzungumza nao kwa kina, akiwaeleza walichokuwa wamekiamua.
“Hiyo dialysis ndiyo nini na inakuwaje?” baba yake Anna alihoji kwani haikuwa mara yake ya kwanza kusikia kuhusu dialysis lakini hakuwa akielewa maana yake halisi, ikabidi Dokta Shivji aanze kumfafanulia.

“Wagonjwa wenye matatizo ya figo, mara nyingi huhitaji kufanyiwa dialysis ambayo ni matibabu ya kutumia mashine inayofanya kazi sawa na figo, kutoa sumu, maji yaliyozidi na taka nyingine katika mwili.

“Katika tiba hii, zipo aina kadhaa za dialysis lakini ambazo ni maarufu zaidi ni mbili; hemodialysis catheter na hemodialysis graft. Katika aina ya kwanza, mshipa mkubwa wa vena unaopitisha damu, hutobolewa eneo la shingoni au kifuani kwa juu kisha mrija mdogo laini (catheter) huingizwa ndani yake ukiwa na sehemu maalum ya kufunga na kufungua.

“Kidonda kikishapona, mrija huo hubaki ndani ya mwili kwa maisha yote ya mgonjwa na anapopelekwa kwa ajili ya damu yake kusafishwa kwenye mashine ya dialysis, mrija huo hufunguliwa na kuruhusu damu kuingia na kutoka kwenye mashine hiyo maalum,” alisema Dokta Shivji, wazazi wa msichana huyo wakajikuta wakisisimkwa mno na maelezo hayo.

Daktari huyo aliendelea na ufafanuzi wa aina ya pili ya dialysis lakini akahitimisha kwamba, aina ya kwanza ndiyo inayotumika zaidi kwa sababu ni rahisi na salama, akaeleza pia kwamba wao kama madaktari walikubaliana kutumia aina hiyo ya kwanza.

Maandalizi yalianza kufanyika, Anna akaingizwa kwenye chumba cha upasuaji mdogo kwa ajili ya kumuingizia mrija huo mdogo (catheter) kwenye mwili wake, zoezi lililochukua muda mfupi kukamilika. Baada ya hapo, Anna aliingizwa kwenye chumba maalum cha dialysis na kwa mara ya kwanza, akafanyiwa tiba hiyo kwa muda wa saa nne mfululizo.

Hatimaye alitolewa kwenye chumba hicho na kurudishwa wodini ambapo alipozinduka usingizini, jambo la kwanza lilikuwa ni kumuulizia Jafet.

“Jafet amebaki Tanzania Anna, si tulishazungumza kwamba kwa sababu mwenzako yupo chuoni na amekaribia kufanya mitihani abaki?” baba yake Anna alizungumza kwa upole na binti yake huyo.

“Baba, nahisi kama maisha yangu yanaelekea ukingoni, nilikuwa nahitaji kuzungumza na Jafet kabla sijafa,” alisema Anna, kauli iliyowafanya wazazi wake watazamane wakiwa ni kama hawaamini walichokisikia.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

2 Comments
  1. mihayo says

    Duuuh nzuri

  2. dorah fredy says

    To late Anna kama ni mimi Jafet nakataa kusafiri bila Shelei

Leave A Reply