The House of Favourite Newspapers

UNESCO Yajenga Kituo cha Malezi, Makuzi ya Watoto Sengerema

0

Sengerema. Shirika la Kimataifa UNESCO kwa ufadhili wa Shirika la Korea (KOICA) kupitia mradi wa kuwawezesha wasichana walio katika umri balehe na akina mama wenye umri mdogo kupitia elimu nchini Tanzania wamejenga kituo cha mfano cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kilichojengwa katika kata ya Mwabaluhi wilayani humo.

 

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa kituo hicho, Mkurugenzi mkazi na Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania, Tirso Dos Santos amesema mradi huu umelenga kuboresha malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wilayani Sengerema hivyo kuweza kumwandaa mtoto kukuwa kiafya, kiakili na kimwili ili kujiandaa vyema pindi ifikapo muda wa kuanza shule.

 

Tirso dos Santos amesema mradi huu kwa Tanzania Bara unatekelezwa kwenye Wilaya tatu za mfano ambazo ni Sengerema, Kasulu na Ngorongoro pekee ambapo katika kila wilaya, UNESCO wamejenga kituo kama hicho. Katika wilaya ya Sengerema, mradi huo unatekelezwa katika kata tano ambazo ni Mwabaluhi, Mission, Nyampulukano, Nyatukala na Ibisabageni.

 

Akihitimisha katika hafula hiyo, ndugu Dos Santos amesema; “Ninawaomba wananchi kuutunza mradi huu na kuwaleta watoto wenye umri kuanzi miaka 2 hadi 4 ili wapate kujifunza katika kituo hiki.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, ndugu Abel Mosha amesema kituo hiki kimejengwa ili kuwa mfano katika jamii inayotuzunguka hasa katika suala la malezi ya watoto. Hivyo ninawaomba wananchi kuwaleta watoto wao ili wapate malezi bora.

 

Afisa Ustawi wa Jamii Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, Nyanjige Julius amesema kituo hiki cha kulea watoto kina uwezo wa kuhudumia watoto wasiozidi 50 hivyo anaiomba jamii kujitokeza kuleta watoto kwenye kituo hicho.

 

Mmoja wa wakazi Wilayani Sengerema, Sarah John amesema kituo hicho kitaisaidia jamii ya Kata ya Mwabaluhi katika suala la malezi ya watoto hivyo tunatakiwa kukitunza na kukithamini ili kiweze kudumu.

 

Gabriela Lucas ambaye ni Mratibu wa mradi wa kuwawezesha wasichana walio katika umri balehe na akimama wadogo amesema mradi huu utakuwa chachu ya maendeleo kwa wanasengerema hivyo wananchi wanatakiwa kuwa na mkakati bora wa kukiwezesha kituo kuendelea ikiwemo kuandaa mpango wa kuchangia gharama za uendeshaji wa kituo hicho.

Daniel Makaka

Leave A Reply