The House of Favourite Newspapers

UNHCR Yamwomba Radhi JPM kwa Kuingiza Nguo Zinazofanana na za Jeshi

KAMISHNA Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Filippo Grandi amemwomba radhi Rais wa Tanzania, John Magufuli kufuatia kukamatwa makontena yaliyoingizwa nchini yakiwa na nguo zinazofanana na Sare za Jeshi.

 

Grand ameomba radhi hiyo jana Jumatano, Februari 6, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.

 

Januari 10, 2019 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ilikamata jumla ya sare 1,947 kwenye kambi ya wakimbizi ya mtendeli na Nduta. Licha ya nguo hizo kuchomwa moto, kamishna huyo amemuahidi Rais Magufuli kuwa jambo hilo halitajirudia.

 

“Ilitokea kampuni moja ya Japan ilitoa msaada wa nguo kwa ajili ya wafanyakazi wetu, nguo zile kwa bahati mbaya zilikuwa zinafanana kama sare za jeshi, na tulizipokea ili tuzisambaze kwenye maeneo ambayo tunawahudumia wakimbizi. Hili ni kosa, hatukupaswa kufanya hivyo na hatujawahi kufanya hivyo, lakini wakati mwingine vitu hivi vinatokea, namuomba radhi Rais na ninamuahidi kuwa haitatokea tena,” amesema.

 

Rais Magufuli amempongeza Grandi kwa uungwana wake wa kuomba radhi kwa kitendo cha kuingiza nguo zinazofanana na Sare za Jeshi na anaamini UNHCR haitarudia kufanya hivyo.

Comments are closed.