The House of Favourite Newspapers

Usajili Yanga Waipa Hofu Simba SC

WAKATI kikosi cha Yanga kikiendelea kujifua huko mkoani Morogoro kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya ametishwa na usajili uliofanywa na klabu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Kakolanya ambaye sasa yupo Afrika Kusini na kikosi cha Simba baada ya kusajiliwa hivi karibuni, alisema kutokana na usajili huo ambao Yanga imeufanya hivi karibuni, anaamini msimu ujao timu hiyo itatisha.

 

Alisema kama wachezaji waliosajiliwa watakuwa na ubora ambao amekuwa akiusikia basi anaamini timu hiyo itatoa upinzani mkubwa kwa timu nyingine za ligi kuu ikiwemo timu yake ya sasa ya Simba.

 

“Niwapongeze tu Yanga kwa usajili walioufanya kwani kwa harakaharaka unaonekana kuwa ni mzuri jambo ambalo linaweza kutoa ushindani mkubwa kwa timu nyingine za ligi kuu ikiwemo timu yangu ya Simba.

 

“Ukitazama kumekuwa na mastaa wakubwa sana ambao wametajwa kusajiliwa na timu hiyo kama mchezaji lazima nijiandae vyema kukabiliana nao.

 

“Kwa hiyo sina mengi ya kusema zaidi ya hilo lakini niwapongeze tu kwa hilo, tukutane uwanjani,” alisema Kakolanya.

 

Alipoulizwa kuhusiana na nafasi ya kipa katika kikosi cha Yanga anaionaje alisema kuwa: “Makipa wote waliosajiliwa Yanga ni wazuri ila ningependa zaidi kuona Ramadhan Kabwili pamoja na Metacha Mnata ndiyo wanakuwa tegemeo katika kikosi hicho.”

Comments are closed.