USIYOYAJUA KUHUSU UGONJWA WA MAFUA

UGONJWA wa mafua unaweza kuwa moja ya sababu kubwa inayofanya watu wengi kushindwa kwenda kazini, shuleni au kwenye shughuli mbalimbali.  Ugonjwa wa mafua unaweza kusababisha hali ya kupiga chafya mara kwa mara, kutokwa na makamasi mepesi au mazito puani, kikohozi, homa kali, na kuziba kwa pua. Dalili zingine ni pamoja na kichwa kuuma, uchovu wa mwili, kupoteza hamu ya chakula na hali ya kukereketa kooni. Dalili hizi huanza ndani ya saa 16 tangu wakati wa kugusana na virusi au visababishi vya mafua.

Hali huwa mbaya katika kipindi cha saa 24 hadi 72 ambapo virusi huwa vingi katika majimaji yatokayo puani. Katika kipindi hiki mgonjwa wa mafua huwa na uwezo mkubwa wa kuambukiza watu wengine. Dalili za ugonjwa wa mafua hutegemea zaidi uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa kuliko uwezo wa virusi kushambulia nyama za mwili katika njia ya mfumo wa hewa.

Mafua yanaweza kusababisha matatizo makubwa katika mfumo wa kupumua hasa pale yanapoambatana na uambukizo wa pili wa bakteria. Matatizo yanaweza kuwa makubwa zaidi kwa watoto wachanga, wazee au kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.

Mafua pia yanaweza kusababisha ugonjwa wa uambukizo wa bakteria katika matundu ya fuvu la kichwa (sinusitis), uambukizo katika masikio na koo. Katika kipindi hiki mgonjwa hutoa makohozi au makamasi yenye rangi ya njano yanayofanana na usaha. Katika hatua hii, mgonjwa wa mafua anaweza kupata homa kali sawa na mtu mwenye homa ya Malaria. Kimsingi mafua yanasababishwa na uambukizo wa virusi vya mafua. Kuna aina zaidi ya 200 za virusi vinavyosababisha mafua ingawa virusi aina ya rhinoviruses vilivyogunduliwa miaka ya 1950, ndivyo vinasababisha mafua kwa kwa asilimia 30 hadi 80.

Aina zingine za virusi vya mafua ni human coronavirus, influenza viruses, adenoviruses, human parainfluenza viruses, human respiratory syncytial virus, enteroviruses na metapne umovirus.Mara nyingi mtu anaweza kupata uambukizo wa virusi vya mafua vya aina mbalimbali kwa kipindi kimoja anapoumwa mafua. Kwa kawaida mafua hutokea zaidi wakati wa mvua na baridi kali. Hii ni kutokana na uwezo wa virusi wa mafua kusambaa kwa kasi wakati wa baridi.

Lakini pia katika kipindi cha baridi kali njia ya hewa katika mfumo wa kupumua, huwa kavu kiasi cha kushindwa kukabiliana na virusi wa mafua kwa ufanisi mkubwa. Mafua pia yanaweza kusababishwa na mzio katika mfumo wa kupumua. Mafua yatokanayo na mzio wa njia ya kupumua ni tatizo la ulimwengu mzima na kwamba utokeaji wa tatizo hili ni asilimia 10 hadi 40 na tatizo hili linaongezeka.

Sababu kubwa zinazochangia kutokea kwa aina hii ya mafua ni uchafuzi wa hewa, vumbi hasa la ndani ya nyumba, moshi wa sigara, hali ya baridi na matumizi ya pafyumu zenye harufu kali. Kwa kawaida mafua yatokanayo na mzio hayaambatani na homa, yanakuwa meupe, mepesi, wakati mwingine yanaambatana na muwasho wa macho, ugonjwa wa pumu au kutokea kwa uvimbe wa vinyama puani (nasal polyps).

Ukavu wa hewa au kupungua kwa unyevu katika hewa, husababisha vinywele (cilia) katika njia ya hewa kushindwa kukamata virusi vya mafua na kuvisafirisha hadi tumboni ambako kwa kawaida huunguzwa kwa tindikali (acid) ya tumboni na kufa. Mwili wa binadamu huwa katika hali bora pale unyevu wa hewa unapokuwa kati ya asilimia 20 na 60.

KUKABILIANA NA MAFUA

Njia zinazosaidia kukabiliana na tatizo la mafua ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kushika shika pua na macho. Ni vizuri kufunika pua na mdomo kwa kitambaa wakati wa kupiga chafya au kukohoa. Watu wanaofanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, hawakabiliwi na tatizo la mafua mara nyingi ikilinganishwa na wale wasiofanya mazoezi.

Kula mbogamboga na matunda kwa wingi pia ni njia bora ya kupunguza uwezekano wa kupata mafua kutokana na kupata vitamin C na madini ya zinki kwa wingi ambayo husaidia kinga ya mwili kukabiliana na virusi.

Toa comment