The House of Favourite Newspapers

Utajiri wa mastaa, Shilole akimbiza mwizi kimya kimya

UTAJIRI wa mastaa mbalimbali Bongo unazidi kukua kila kukicha ambapo mwanamuziki anayetamba na ngoma ya ‘Nikagongee,’ Zuwena Mohammed ‘Shilole’ naye anakimbiza mwizi kimyakimya kutokana na vitu anavyovimiliki. 

 

Risasi Jumamosi lilimfungia kazi Shilole ili kujua utajiri alionao kwa sasa kwani amekuwa kati ya wanawake wapiganaji Bongo ambapo aliweka wazi baadhi ya mali zake na nyingine akisema ni siri yake.

 

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Risasi Jumamosi, Shilole alisema anamshukuru Mungu kwa mali anazomiliki kwani ameweza kujenga nyumba kwa mkono wake kupitia muziki na kazi yake ya kupika.

 

“Unajua nimepitia magumu mengi lakini namshukuru Mungu amenipa mali japo siyo nyingi sana kwa njia ya halali kwani kama mnavyoona nimefanikiwa kujenga nyumba nzuri kwa gharama kubwa japo mpaka sasa sikumbuki nimetumia shilingi ngapi lakini kwa wanaojua kuthaminisha majengo wataelewa nimeteketeza bei gani,” alisema Shilole.

 

Mali nyingine alizozitaja kumiliki Shilole ni pamoja na ghorofa ambalo ameanza kulijenga hapohapo nyumbani kwake maeneo ya Majohe, Dar kwani anamiliki uwanja mkubwa pembeni ya nyumba anayoishi aliyohamia mwaka jana baada ya kumaliza ujenzi wake.

“Nimeanza kujenga ghorofa ambayo nitaishi na mume wangu na nyumba ninayoishi kwa sasa watakaa watoto na ndugu zangu wengine,” alisema Shilole.

 

Mwanamama huyo aliongeza kuwa mbali na nyumba, pia anamiliki shamba la heka tano lililopo Mkuranga, Pwani ambapo analima pilipili anazosaga na kuuza, gari aina ya Toyota Harrier ambayo thamani yake ni shilingi milioni 30, pikipiki tatu ambazo ni kwa ajili ya kusambazia chakula.

“Nikitaja mali zangu huwa napendelea kutaja hata mgahawa wangu ninaoumiliki, ambao ni sehemu ya mali zangu kwani umeniwezesha kupata vitu mbalimbali ninavyovimiliki, kwa ujumla. Mgahawa umenipa mafanikio kwani nimeweza pia kutoa ajira kwa wafanyakazi kumi na tano,” alisema Shilole.

 

Shilole alimalizia kwa kusema kuwa mbali na mali hizo alizozitaja, pia anamiliki gari lingine aina ya Toyota Noah inayomsaidia kupeleka wafanyakazi kwenye tenda mbalimbali za kazi hasa anapopata tenda za kwenye shughuli kama harusi na nyinginezo kubwa.

 

“Namiliki Toyota Noah ambalo nilipewa na msanii mwenzangu ambaye ni kaka yangu, Rajab Khan ‘Harmonize’ ambaye bila yeye kunipa pesa nisingeweza kuimiliki, alinipa pesa kama zawadi kwenye harusi yangu ambapo nilinunua gari aliyokuwa ameidhamiria,” alisema Shilole.

Tujikumbushe

Shilole alianza kupata umaarufu kupitia filamu za Kibongo akapambana na kuamua kuachana na filamu na kuhamia kwenye muziki lakini hakuishia hapo aliingia kwenye ujasiriamali kwa kuanza na kufungua baa, baadaye akahamia kwenye mgahawa unaojulikana kwa jina la Shishi Food unaompatia mkwanja mpaka sasa.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi

Comments are closed.