The House of Favourite Newspapers

Chadema Yapata Pigo Tena

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepata pigo jingine baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Njombe Edwin Enosy Swale (wakili) kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Akizungumza mara baada ya zoezi la kupokelewa, kuapishwa na kukabidhiwa kadi ya CCM katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Njombe, amesema amefanya maamuzi hayo kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli katika maendeleo nchini.

 

“Mimi kama kijana nimeamua kwa dhati kutumikia nchi yangu katika chama ambacho kwa sasa kimekuwa na muelekeo wa kusaidia wananchi, na nitoe wito kwa vijana wote nchini na Watanzania kwa ujumla wake, tusije tukapoteza fursa ya kutokumtumia Magufuli kuipeleka nchi yetu katika hali neema,” alisema Swale.

 

Swale alikuwa Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya hiyo baada ya Mwenyekiti wa awali, Fakih Lulandala, kukihama chama hicho mwaka jana 2018 na kujiunga na CCM.

 

Katika hatua nyingine CCM imempokea aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) Jimbo la Lupembe, Msafiri Peter Mpolo, ambaye amesema ameamua kuhama chama hicho kutokana na kutokuwepo kwa ajenda za kusimamia kwa sasa.

 

“Tumeona hakuna sababu ya kuendelea kuwa chama cha upinzani kutokana na mambo makubwa ambayo yamefanywa na serikali kwa sasa, ukienda Makete utaona barabara zinavyojengwa, watumishi wamekuwa na nidhamu kubwa, hizo ndio ajenda tulizokuwa tunasimamia lakini leo hii nikibaki Chadema nitasimamia nini?” alisema Mpolo.

 

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha na kuwakabidhi kadi wanachama hao,  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Edward Mgaya, amemtaka Swale kuunganisha nguvu zake pamoja na Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Jorum Hongoli,  ili kufikisha maendeleo katika jimbo hilo.

Comments are closed.