The House of Favourite Newspapers

Utu Kwanza Waja Na Miradi Ya Usaidizi wa Kisheria, Serikali Yawapongeza

0
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul (mwenye mkasi) akikata utepe kuashira uzinduzi huo.

Dar es Salaam 10 Septemba 2023: Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul ameipongeza Taasisi ya Utu Kwaza kwa kuzindua miradi mbalimbali ya kisheria ikiwemo mradi wa nyumba salama ambao utawasaidia watoto ambao wazazi wao wako gerezani na kuwasaidia wamama wanaojifungua wakiwa gerezani kwa kumsaidia huyo mtoto kwakuwa watoto hao wakitelekezwa wanaingia mitaani.

Uzinduzi huo umefanyika katika mbio maalum zilizoitwa Utu Kwanza Run za kilometa 60 zilizoanzia Bagamoyo, Pwani na kuishia Viwanja vya Leaders Club zikiwashirikisha watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul akimpongeza Mwenyekiti wa Utu Kwanza, Wakili Shehzada Amir Walli kwa uzinduzi mradi huo unaotarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa jamii.

Katika mbio hizo pia kulikuwa na mbio fupi za kilometa tano kwa ajili ya watoto na waliotaka kujifurahisha nazo.

Akizungumza baada ya mbio hizo Mwenyekiti wa Utu Kwanza Wakili Shehzada Amir Walli amesema lengo la hafla hiyo ni uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kisheria ikiwemo mradi wa nyumba salama ambao utawasaidia watoto ambao wazazi wao wako gerezani.

Wakili Shehzada amesema mradi huo pia utawasaidia wazazi wanaojifungua wakiwa gerezani kwa kumsaidia mtoto kwa maana watoto wanapotelekezwa mara nyingi huingia mitaani na kuishia kuwa waalifu.

Mwenyekiti huyo wa Utu Kwanza amesema mradi huo wa nyumba salama unatarajiwa kuanzishwa mapema mwakani kwenye Februari mpaka Machi.

Ifuatayo ni risala ya Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul kwenye hafla hiyo;

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul, Mwenyekiti wa Utu Kwanza, Wakili Shehzada Amir Walli na wadau wengine wakiwapokea waendesha baiskeli waliokimbia kilometa 60 kutoka Bagamoyo.

“Waheshimiwa Viongozi au Wawakilishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mliopo hapa; Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; Mh. Mbunge wa Kinondoni/Mwakilishi wake; Mwenyekiti na Bodi ya Wakurugenzi ya Utu Kwanza; Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Ofisi ya Mkoa wa Kipolisi – Kinondoni; Viongozi na Wawakilishi kutoka Jeshi la Magereza; Taasisi binafsi Wadau wa Haki na Msaada wa Sheria Nchini mliopo hapa; Wageni Maalum waalikwa Meza Kuu; Wakimbiaji, Watembeaji na Waendesha Baiskeli walioshiriki “Utu Kwanza Run” leo hii, Wadhamini (Sponsors); Vjina kwa Wazee Waliojitolea kufanikisha siku hii ya leo (yaani Volunteers); Wanahabari na Ndugu Wananchi wote kwa ujumla, nawasalimu – JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA! …….. (Kazi Iendelee!)

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Gekul, akipasha na wakimbiaji baada ya kuwasili Viwanja vya Leaders.                                                                                                                                                           Kwa niaba ya Waziri wa Sheria na Katiba nchini, Mh. Pindi Chana (Mb), nianze kwa kuwashukuru sana Vijana Wanasheria wa Kitanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Utu Kwanza, Wakili SHEHZADA AMIR WALLI na Bodi yote ya Wakurugenzi ya Utu Kwanza kwa kubuni na kujitoa kwa hali na mali (hasa muda wenu) ili kutekeleza jukumu adhimu kabisa la kuboresha Maisha ya Mahabusu na Wafungwa, familia za hao Mahabusu na Wafungwa, na hata kwenda mbali zaidi na kuangalia namna bora ya kuboresha Maisha ya Maofisa wa Magereza wanaoishi na kuwajibika moja kwa moja na usimamizi wa Mahabusu na Wafungwa Nchini. HONGERENI SANA!

Sisi kama Wizara, nitumie Jukwaa hili kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuingoza Serikali ya Awamu ya Sita kwa umakini kabisa akiweka “Utu” na “Maslahi” ya Watanzania mbele hasa katika masuala mazima ya Utoaji na Upatikanaji wa HAKI Nchini. Sote tu mashuhuda, ni hivi karibuni Serikali ya Mama yetu SAMIA, iliunda tume maalum ya kupitia na kutoa mapendekezo ya kurekebisha mfumo.

wa haki jinai nchini Tanzania, maarufu kama TUME YA JAJI OTHMAN CHANDE (Jaji Mkuu Mstaafu), ambayo imefanya kazi kubwa kwa kuzunguka Nchi nzima (Bara na Visiwani) ikikusanya Mawazo kwa Wananchi na Wadau wote wa Sheria ili kuboresha Mfumo mzima wa Haki Jinai Nchini. Ndio maana, sisi kama Wizara ya SHERIA NA KATIBA, hatukusita kupokea wito na kushiriki kwenye Hafla hii ya Utu Kwanza baada ya kuridhishwa na Malengo na kazi nzuri inayofanywa na Shirika hili la Utu Kwanza sambamba na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha Maisha ya Watanzania wote bila kujali rangi, itikadi, jinsia wala asili kwenye Sekta ya Upatikanaji wa HAKI, na hasa HAKI JINAI – ambako ndiko linapopatikana Kundi la MAHABUSU na WAFUNGWA.

Utu Kwanza, jina hili limebeba maana kubwa na pana sana; kwa kifupi, linamaanisha “Ubinadamu Kwanza”. Ni matarajio ya Wizara na Serikali kwa ujumla kuona kuwa Shirika hili linaendeleza malengo yake kwa mujibu wa Sheria za Nchi, katika kulinda na kuboresha “utu” na thamani ya Binadamu katika upatikanaji wa haki Jinai. Ni rai yetu kama Wizara, wadau mbali mbali wa Sheria na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha Msaada wa Sheria Nchini kutumia rasilimali zake vizuri ili kuwafikia walengwa na kushirikiana na Serikali katika kuboresha Maisha ya watu wote. Utu uendelee kuwa kipaumbele chetu kwenye HAKI JINAI na sote tutatimiza wajibu wetu katika kuwatumikia Watanzania na kudumisha Amani na Mshikamano ambazo ni tunu muhimu kwa Maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Wizara ya Sheria na Katiba inatambua na kuthamini mchango mkubwa na jitihada za Shirika la Utu Kwanza katika kuboresha maisha na “Utu” wa Wafungwa na Mahabusu katika kipindi cha miaka Sita (06) tangu kuanzishwa kwake kwa kuwafikia Mahabusu na Wafungwa katika baadhi ya Magereza hapa Nchini, hasa Jijini Dar es Salaam; HONGERENI SANA! Leo, kwa kuanzisha Mradi wa DAWATI LA MSAADA WA SHERIA, (yaani, LEGAL AID DESK) mnapata sababu nyingine ya kusherehekea mafanikio makubwa ya kazi yenu katika kuweka maslahi ya “Utu Kwanza” kwa vitendo. Tukio hili la Utu Kwanza Run halisaidii tu afya na kuwaleta Wanajamii pamoja, bali pia nimeambiwa linasaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya Mradi wa

Dawati la Msaada wa Kisheria, (“Legal Aid Desk”). Mradi huu ukisimamiwa vizuri, utakuwa ni jawabu zuri kwa Umma na Watanzania walio wengi wanaohitaji Msaada wa dharura hasa pale wanapopatwa na matatizo ya Kijinai. Watanzania na Jamii, watumie fursa hizi vizuri ili watu wasio na uwezo wa kupata msaada wa kisheria kwa gharama za kulipia, wapate msaada unaostahili.

Mwisho, lakini si kwa umuhimu, napenda kutoa pongezi za pekee kwa Mwenyekiti wa Utu Kwanza, Ndugu Shehzada Walli, na washiriki Zaidi ya 10 wa “Utu Kwanza Run” ambao wameonyesha ujasiri mkubwa na uthubutu wa kukimbia umbali wa kilomita 60 kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam. Hii inaonesha wazi dhamira yao na shauku ya kukamilisha Malengo muhimu ya Utu Kwanza, HONGERENI SANA!

Nitoe pia wito kwa Mahakama kuona ni namna gani wanaweza kushirikiana na Utu Kwanza katika kusaidia upatikananji wa msaada wa kisheria kwa Wahitaji, kupitia Mradi huu wa “Legal Aid Desk” yaani “Dawati la kutoa Misaada wa Kisheria” ambalo nimeambiwa litafanya kazi vizuri likipata nafasi katika Mhakama zetu, ambako ndiko wahitaji (Mahabusu na Wafungwa) wanafikishwa mara kwa mara. Nimeambiwa Mradi huu umeomba “Pilot Project” ifanyike pale Mahahakama ya Wilaya Kinondoni, namuomba Mheshimiwa Jaji Mkuu na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama na Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, kuangalia namna ya kusaidia utekelezaji wa Mradi huu kwa mashirikiano na Mahakama, bila kuathiri taratibu zingine za Utendaji na Utoaji wa haki, hasa HAKI JINAI.

Nawashukuru tena wote kwa kushiriki katika tukio hili muhimu, na Nitamke rasmi kuwa MRADI WA DAWATI LA MSAADA WA SHERIA (The LEGAL AID DESK) wa Utu Kwanza sasa Umezinduliwa rasmi! KAZI IENDELEE!

Leave A Reply