The House of Favourite Newspapers

VIDEO: MAGUFULI AZINDUA MRADI WA STIEGLER’S GORGE

Rais John  Magufuli.

RAIS John  Magufuli leo Ijumaa,  Julai 26, 2019,   amezindua mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge utakaotoa megawati 2115 kutokana na maji ya  Mto Rufiji mkoani  Pwani.

 

Mradi huu  umelenga kuzalisha umeme kwa ajili ya kutekeleza malengo  ya maendeleo nchini  ambapo kampuni zinazohusika na ujenzi ni kutoka Misri.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika uzinduzi huo, umeme huo utasafirishwa kutoka Rufiji kwenda Chalinze, Dar es Salaam hadi Dodoma na ndiyo umeme utakaotumika katika kuendesha treni ya mwendokasi.

 

Katika hotuba yake ya uzinduzi, amesema mradi huo utasaidia katika juhudi za kujenga uchumi wa viwanda nchini kwani utakuwa ni umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

 

“Mradi huu utazalisha umeme mwingi ambao ni mwingi kuliko umeme wote uliozalishwa nchini Tangu tumepata uhuru, tutakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wa bei nafuu,” alisema na kuongeza kwamba utasadia kikamilifu  kukuza sekta ya biashara na uwekezaji nchini.

Pia aliagiza  barabara kutoka eneo la Fuga hadi eneo la mradi ijengwe kwa kiwango cha lami akisema fedha itakayotumika kwa kazi hiyo ni ile iliyorudishwa nchini kutoka Kenya baada ya kutoroshwa na kuibiwa hapa nchini, yakiwemo madini.

 

“Ninaagiza barabara kutoka eneo la Fuga mpaka eneo la mradi ijengwe  kwa kiwango cha lami, na tutatumia fedha zilizorudishwa na ndugu yetu  Rais Uhuru Kenyatta,” alisisitia na kuongeza kwamba ugavi wa umeme nchini umefikia vijiji 7,419 na kwamba hilo ni ongezeko la asilimia 254 katika juhudi za kuwafikishia wananchi umeme.

Akitoa uchambuzi mbalimbali wa mradi huo, alisema bwawa likikamilika liitwe Bwawa la Nyerere na kwamba sehemu ya hifadhi ya Selous Game Reserve itakayokatwa iitwe Nyerere National Park.

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliusifia mradi huo akisema utakamilisha ndoto za serikali ya awamu ya tano ya kufikisha umeme kwenye kila nyumba ya Mtanzania “bila kujali kama ni nyumba ya tembe”.

 

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa  serikali na taasisi, wakiwemo mabalozi na wataalam wa masuala ya umeme.

Comments are closed.