The House of Favourite Newspapers

Vifaa Vipya Yanga Kuanza Kutua Julai Aziz Ki, Bernard Morrison, Adriano Ndani

0

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa wachezaji wao wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu ujao, rasmi wataanza kutua nchini Julai 3, mwaka huu.

 

Hiyo ni katika kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga itaiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo mikubwa Afrika.

 

Kati ya wachezaji wanaotajwa kumalizana na Yanga katika usajili ni Stephane Aziz Ki, Bernard Morrison, Adriano Belmiro (Yano) na Lazarus Kambole ambaye yeye ametambulishwa tayari na timu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa timu hiyo, Injinia Hersi Said, alisema kuwa mara baada ya mchezo wa Fainali ya Kombe la FA, Julai 2, mwaka huu kesho yake wataanza kutambulisha wachezaji wapya wa kigeni waliowasajili.

 

Hersi alisema kuwa lengo la kuwatambulisha wachezaji hao mapema ni kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michuano ya kimataifa kwa kwenda kuweka kambi nje ya nchi ambako ni Boston, Marekani.

 

Aliongeza kuwa kikubwa wanataka kufanya vema katika michuano hiyo mikubwa Afrika ambayo malengo yao ni kufika mbali zaidi.

 

“Mara baada ya kumtambulisha Kambole tukafikia makubaliano ya vongozi ya kusimamisha kwa muda utambulisho wa wachezaji wapya kwa lengo la kuelekeza nguvu katika ubingwa wa ligi ambao tayari tumeuchukua.

 

“Hivi sasa tunaelekeza nguvu katika FA, hivyo kila kitu kinachohusiana na usajili tumekisimamisha kwa muda, hivyo tumepanga kuanza utambulisho wa wachezaji wapya wa kigeni mara baada ya mchezo wa fainali ya FA ambao utachezwa Julai 2, mwaka huu.

 

“Baada ya mchezo huo kuanzia kesho yake tutawatambulisha wachezaji hao mara baada ya kutua nchini tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya pre season,” alisema Hersi.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply