The House of Favourite Newspapers

Vijana Hawa Watapata Tabu

0

MCHAKATO wa uteuzi wa wagombea ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umefikia tamati Agosti 20 mwaka huu kwa kushuhudia baadhi ya sura mpya za vijana zikichanua, huku wimbi kubwa la wengine machachari wa chama hicho, wakipewa kisogo.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, John Magufuli kufyeka sura maarufu za vijana ambao sasa watasubiri huruma yake ili kuweza kupenya katika nafasi nyingine zitokanazo na utashi wa kisiasa.

 

Hata hivyo, vijana hao ambao bado wanasafari ndefu kisiasa, kutoswa kwao, pia kumechangiwa na ukaidi waliouonesha licha ya kuonywa na Rais Magufuli kwamba, wasikimbilie kugombea ubunge ilhali wakiwa na vyeo vingine kama ukuu wa mkoa na wilaya.

 

Onyo hilo limegeuka kuwa shubiri kwa baadhi ya vijana maarufu ndani ya chama hicho, kama vile Paul Makonda, David Kafulila na Sophia Mjema.

 

Licha ya kwamba halmashauri kuu ya chama hicho, haikuweka wazi sababu za kuwatosa vijana hao, baadhi ya mambo yaliyotajwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole, ni tuhuma za rushwa.

 

MAKONDA

Paul Makonda licha ya kuwa mmoja wa vijana maarufu ndani ya CCM, pia alijijengea jina nchi nzima kutokana na umachachari katika utendaji wake ambao ulitoa nafasi kung’ara zaidi kwenye vyombo vya habari.

 

Makonda alikuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, nafasi ambayo alipatiwa na Rais John Magufuli, baada ya kufikia mchakato wa kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa ndani ya CCM, aliwania jimbo la Kigamboni na kuangushwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Faustine Ndungulile katika mchakato wa kura za maoni.

 

NASSARI

Joshua Nassari naye ni kijana machachari ambaye alihudumu katika jimbo la Arumeru Mashariki kipindi akiwa Chadema, lakini mwanzoni mwa mwaka huu, alifutiwa ubunge wake na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na utoro ambao sababu zake zilikuwa na walakini.

 

Hata hivyo, kijana huyo msomi ambaye hivi karibuni amehitimu Shahada ya Uzamili ya Sera ya Maendeleo huko nchini Marekani, alirejea kuwania jimbo hilo kupitia CCM, lakini aliangushwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dk. John Pallangyo.

Nassari bado anatazamwa kuwa na safari ndefu kisiasa hususani kutokana na wimbi la vijana waliohamia CCM hivi sasa kusubiri uteuzi wa Rais Magufuli.

 

KAFULILA

David Kafulila ambaye ni mmoja wa vijana walio‘cross’ kutoka upinzani kuelekea CCM na kupata ‘shavu’ baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, naye aliangukia pua katika mchakato wa kura za maoni katika Jimbo la Kigoma Kusini.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Husna Mwilima, alifanikiwa kupita katika mchakato wa kura za maoni na baadaye Halmashauri kuu.

 

MTULIA

Maulid Mtulia naye ni mmoja wa vijana waliohamia CCM, na kupewa nafasi ya kuendelea na ubunge hadi ungwe ya kwanza ilipoisha.

Hata hivyo, katika kura za maoni ndani ya chama hicho, Mtulia aliangushwa na Tarimba Abbas ambaye ndiye mgombea ubunge wa jimbo hilo la Kinondoni.

 

LIJUALIKALI

Peter Lijualikali naye alitoka Chadema na kuhamia CCM katika dakika za mwisho akiwa mbunge wa Kilombero.

Kijana huyo aliangushwa vibaya katika kura za maoni CCM baada ya kuambulia kura tano katika mchakato wa kumpata mgombea ubunge, ambapo Aboubakar Assenga ndiye aliyenyakua jimbo hilo.

Hata hivyo, Lijualikali hakukata tamaa na kurejea kugombea udiwani ambalo nako alishindwa baada ya kupata kura mbili.

 

MGIMWA

Aliyekuwa mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa naye alitupwa katika kura za maoni na hatimaye katika uteuzi, Halmashauri Kuu ikampatia Jackson Kiswaga ambaye sasa atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

 

MLINGA

Goodluck Mlinga ambaye alikuwa mbunge machachari bungeni kutokana na hoja zake zilizokuwa zimejaa kebehi na vijembe dhidi ya wapinzani, safari hii Watanzania watakosa uhondo wake baada ya kuangushwa na Salim Hasham. Hasham alimshinda Mlinga katika kura za maoni na baadaye katika uteuzi, Halmashauri Kuu haikufanya ajizi na kumrejesha Mlinga kijiweni.

 

BULEMBO

Si wabunge wa majimbo pekee, hata wa viti maalumu pia walionja shubiri akiwamo Halima Bulembo aliyekuwa Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Kagera akiwakilisha vijana.

 

Halima ambaye ni mtoto wa kada maarufu wa anga la siasa nchini; Abdalah Bulembo, naye aliondolewa kwenye nafasi hiyo licha ya kushinda katika mchakato wa kura za maoni mkoani humo.

 

KAMATA

Vick Kamata ambaye awali alikuwa mbunge wa viti maalumu, naye alijitosa katika jimbo la Kibamba, lakini aliangushwa katika mchakato wa kura za maoni na Issa Jumanne Mtemvu ambaye sasa Halmashauri Kuu ya CCM imemteua kuwa mgombea ubunge.

 

MWANJELWA

Dk. Marry Mwanjelwa alikuwa mmoja wa manaibu mawaziri katika Serikali ya awamu ya tano, naye aliangukia pua katika mchakato wa kura za maoni viti maalumu huko mkoani Mbeya. Hata hivyo, tuhuma za kugawa rushwa zinatajwa kumuangusha baada ya kuvuja sauti akigawa fedha kwa baadhi ya wajumbe wa chama hicho.

 

SERUKAMBA

Licha ya kuwa mbunge kwa Kigoma Mjini kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, na baadaye Kigoma Kaskazini mwaka 2015 hadi 2020, kijana huyo mzoefu wa siasa aliangushwa na Asa Nelson Makanika.

Makanika anadaiwa kunyakua nafasi hiyo baada ya Serukamba kukumbwa na tuhuma za rushwa kwenye mchakato wa kura za maoni jambo ambalo linadaiwa pia kuchangia anguko lake.

 

MJEMA

Licha ya kuwa mkuu wa wilaya ya Ilala mwenye bashasha la kipekee, vilevile katika utendaji wake, Sophia Mjema naye alikuwa mmoja wa watumishi walioweka sikio kando kuhusu kauli ya Rais Magufuli na kwenda kugombea jimbo la Ilala.

Hata hivyo, Mjema aliangushwa katika kura za maoni na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mussa Zungu na sasa ndiye aliyeteuliwa kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo.

 

OBAMA

Albert Obama alianza kutikiswa bungeni baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kutangaza kuwa atakwenda kugombea jimbo hilo.

Na ndivyo ilivyokuwa baada ya Dk. Mpango kumwangusha Obama katika kura za maoni na baadaye kuteuliwa na Halmashauri kuu ya chama hicho kuwa mgombea ubunge.

Mbali na vijana hao, wengine waliotoswa katika nafasi hiyo ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Handeni vijijini; Mboni Mhita, Ezekiel Maige (Msalala) na Allan Kiula (Iramba Mashariki).

 

WACHAMBUZI: WASITUKANE WAKUNGA…

Wakizungumza na UWAZI kwa nyakati tofauti baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitoa mbinu mbili za kuwawezesha vijana hao waliotoswa ili waweze kuendelea kung’ara katika medani za siasa.

 

Mchambuzi mashuhuri, Deusi Kibamba alisema ili kupata nafasi za uteuzi baada ya uchaguzi mkuu iwapo CCM itashinda, vijana hao wanapaswa kushiriki ipasavyo kwenye kampeni za wagombea ubunge walioteuliwa na chama hicho.

 

“Waswahili husema, usitukane wakunga na uzazi ungalipo, kwamba wasianze kutukana viongozi wa CCM kwa sababu nafasi uteuzi zaidi ya 600 bado zipo, hivyo watulie na kushiriki vema shughuli za chama.

 

“Kusema ukweli CCM imejipanga sana kwa kubadili mbinu na sasa tumeona sura mpya nyingi ambazo natarajia pia kuziona bungeni kwa sababu vyama vya upinzani havina mbinu mbadala wa kuiondoa CCM madarakani.

 

“Kwa hiyo, kwa kuwa wapiga kura hupendelea kuona sura mpya za wawakilishi wao majimboni, upo uwezekano mkubwa wa vijana wapya hao kushinda ubunge,” alisema.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa ambaye alisema huu ndiyo muda wa vijana hao waliotoswa kukaa kutafakari na kujipanga kwa kasi katika uchaguzi wa mwaka 2025.

 

“Mbali na kwamba sasa wanapaswa kujiwekeza kwenye shughuli nyingine kama za kilimo, lakini pia waandae mikakati imara ya kuwafanya waweze kupenya ifikapo mwaka 2025,” alisema.

MWANDISHI WETU, UWAZI

 

Leave A Reply