Viongozi Sita wa CCM Wafariki kwa Ajali ya Gari eneo la Ndulamo
Viongozi sita wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamefariki dunia kwa ajali ya gari eneo la Ndulamo wakati wakitoka kwenye mkutano wa mlezi wa chama hicho Mkoa wa Njombe, Halima Mohamed Mamuya uliyokuwa ukifanyika wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe John Makuri Imori amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Ndulamo “Gari Namba T 733 BBP aina ya Toyota Hiece likiwa linatokea Makete kuelekea Tandala likiwa na abiria 18 lilipata ajali kwenye kona likapinduka na kuanguka na baada ya ajali kutokea Watu 6 wamefariki (Watatu Wanaume na watatu ni Wanawake), chanzo cha ajali ni mwendokasi na Dereva akashindwa kulimudu gari hilo na kulikuwa na mteremko”
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga amesema majeruhi wengi wamevunjika viungo na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Ikonda na wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makete ambapo pia tayari Madaktari wengine kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe wamefika katika Hospitali hizo kuongeza nguvu.