Vodacom Tanzania Kugawa Bonasi ya Bil 25 Kwa Wateja Wake Kupitia M-Pesa
Wateja wapatao milioni 11 wa Vodacom Tanzania wanaotumia huduma ya M-Pesa kuanzia leo wataanza kupatiwa mgao wa bonasi kutoka kwenye fungu la shilingi bilioni 25 zilizohifadhiwa kwenye akaunti maalumu ya M-Pesa kwenye mabenki mbalimbali nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao alisema, “Mgao wa fedha hizi kwa wateja wetu ni mwendelezo wa kugawa fedha za bonasi ya M-pesa ambao ni utaratibu wetu. Hapo awali tuligawa takriban bilioni 20; awamu hii inayoanza leo tutagawa bilioni 25 na kuanzia sasa tutakuwa tunatoa gawio kila baada ya kipindi cha miezi mitatu” alisema Ferrao.
Ferrao alisema “kiasi cha fedha atakachopata mteja kwenye mgao wa fedha hizi utategemea matumizi yake ya huduma hii katika kufanya miamala mbalimbali ya malipo ikiwemo kutuma fedha. Natoa wito kwa wateja wetu ambao wameacha kutumia kadi zetu za simu wakati waliwahi kutumia huduma hii wajiunganishe tena kwenye mtandao wetu ili fedha za mgao wao zisipotee bure. Pia wateja wetu wanaotumia huduma hii kuanzia leo wanaweza kuangalia fedha watakazojipatia kwa kutuma ujumbe wa maneno kwa kuandika neno KIASI na kuutuma kwenda namba 15300”
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa M-Commerce wa Vodacom Tanzania, Sitoyo Lopokoiyit, amesema kuanzia mwezi uliopita imepunguza viwango vya makato kwa watumiaji wa huduma ya M-Pesa kwa miamala ya hadi shillingi 40,000 kwa asilimia 40% hali inayoleta unafuu kwa wateja na mawakala kuendelea kujipatia faida ya kutoa huduma “M-Pesa imeleta mapinduzi makubwa ya huduma za kifedha nchini ikiwa na mtandao wa mawakala zaidi ya 85,000.