The House of Favourite Newspapers

Vodacom Waipongeza Simba Kwa Ubingwa VPL

0

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, PLC, ambayo ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), wameipongeza timu ya Simba kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu wa 2019/2020, ikiwa ni muda mfupi baada ya kukabidhiwa taji la ubingwa huo juzi Jumatano.

 

Mbali na hilo, pia Vodacom imezipongeza timu zote zilizoshiriki VPL msimu huu wa 2019/20.“Tunajivunia sana kuwa sehemu ya Ligi Kuu Bara kwani inaendelea kukua na kuboreshwa mwaka hadi mwaka.

Pongezi zetu pia ziwaendee viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi, klabu zote shiriki, waandishi wa habari, wadhamini wenza pamoja na Watanzania wote kwa jumla kwa kushiriki kikamilifu katika ligi kuu,” alisema Linda Riwa ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Kampuni ya Vodacom.

 

Linda alisema soka ni mchezo pendwa na muhimu hapa nchini na duniani kote. Inaaminika ndiyo wenye idadi kubwa ya mashabiki kuliko michezo zote.

 

Udhamini wa Vodacom katika VPL ni katika kuwapa burudani wateja wa kampuni hiyo na Watanzania kwa jumla, kutoa nafasi za ajira kwa wachezaji na watendaji pamoja na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa jamii na nchi tofauti.

Mtandao wa Vodacom umekuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha na kuwaleta pamoja Watanzania kupitia mtandao namba moja na wenye kasi zaidi hapa nchini. Vodacom inasifika kwa kutoa huduma bora zaidi za data, kupiga simu, SMS na M-Pesa.

 

“Kama mnavyojua mpira wa miguu ni fursa kubwa ya ajira kwa vijana na tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya mafanikio tunayoyaona kutokana na udhamini wetu ambao umewezesha baadhi ya wachezaji kama Mbwana Samatta na Simon Msuva kupata fursa za kucheza nchi za nje na kufika Ulaya,” alisema Linda ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

 

Vodacom kama wadhamini wakuu wa ligi kuu wametoa hamasa kwa klabu zote kuendelea kuwa mabalozi wazuri na kuwaelezea nia ya kuendelea kutoa hamasa na ushirikiano kwetu kuendeleza michezo na hasa soka.

 

Vodacom pia inatoa shukrani za dhati kwa Watanzania kwa kuendelea kujitokeza kushabikia timu zao maana mchezaji wa 12 katika timu yoyote ya mpira ni mashabiki.

 

“Shukrani zetu kwa waandishi wa habari kwa mchango mkubwa wa kuwahabarisha wapenzi wa soka walio ndani na nje ya nchi na kutangaza ligi yetu ya Vodacom Premier League,” aliongeza Riwa.

 

Simba ilikabidhiwa taji hilo juzi baada ya mchezo dhidi ya Namungo, juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Leave A Reply