The House of Favourite Newspapers

Waandaaji Kili Marathon Waonya Kuhusu Uchelewaji Kuchukua Namba

0

WAANDAAJI wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon wamewakumbusha washiriki kuzingatia muda uliotolewa wa kutoa namba za kukimbia huku zoezi hilo likianza Moshi leo.

Hii imetokana na baadhi ya washiriki kufika katika vituo vya kutolea namba wakiwa wamechelewa na kutaka waghudumiwe wakati muda umeshakwisha.

Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager Wadhamini wa mbio hiyo, Irene Mutiganzi.

 

 

“Tulishuhudia jambo hili wakati wa zoezi la Dar es Salaam pamoja na Arusha na muda uliotolewa ulikuwa unatosha kabisa. Lakini baadhi ya washiriki walichelewa sana na hawakuweza kuhudumiwa kwa sababu tulikuwa tumefunga tayari,” walisema waandaaji hao.

Waandaaji hao pia walisisitiza kuwa mara tu muda uliotolewa kwa ugawaji wa namba kwa mji wa Moshi ukiisha zoezi hilo halitaendelea tena.

Mkurugenzi Mtendaji wa Executive Solution waratibu wa mbio hiyo, Aggrey Marealle.

 

 

Kwa Moshi namba hizo zitatolewa katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Ushirika Alhamisi Februari 24, 2022 kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni, Ijumaa Februari 25, 2022 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni na Jumamosi February 26, 2022 kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.

Waandaaji hao walisema mshiriki anaweza kumtuma mwakilishi amchukulia namba lakini lazima awe na nakala ya kitambulisho na ujumbe wa uthibitisho aliolipia kutoka Tigo.

“Washiriki waliojisajili wanatakiwa kuzingatia muda wa zoezi hili katika vituo husika ili kuepusha usumbufu na zoezi likishafungwa hakutakuwa na ugawaji wa namba siku ya mashindano,” walisema waandaaji hao.

Waliongeza kuwa usajili kwa ajili ya mbio za kilomita 5 bado unaendelea kwa kulipia fedha taslimu katika vituo vya kutolea namba.

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2022 ni Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).

Wadhamini wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na Surveyed Plots Company Ltd (SPC) na Bodi ya Utalii (TTB).

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo zimeandaliwa na taasisi ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa na wadau wa hapa nchini kampuni ya Executive Solutions Limited.

Leave A Reply