The House of Favourite Newspapers

Waandishi wa Habari Waaswa Kutumia Kalamu Zao Kutangaza Mazuri ya Nchi

0
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Nchini uliofanyika Millenium Tour jijini Dar.

 

Dar es Salaam, 6 Disemba 2022: Wanahabari nchini wameaswa kutumia kalamu zao kutangaza mema ya nchini na kuachana na habari za upotoshaji kama wafanyavyo wasiolitakia mema taifa letu. Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akifanya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC).

Sehemu ya wanachama kutoka mikoa mbalimbali wakiwa makini kwenye mkutano huo.

 

Msigwa amesema waandishi wa habari wanatakiwa kufanya kazi zao kwa weledi katika kutafuta habari na kuchakata taarifa zilizo sahihi, mfano kumekuwa na upotoshaji katika mabehewa yaliyonunuliwa na serikali, ametokea mtu akaweka mtandaoni na kusema kuwa siyo mapya, sasa kama siyo mapya aende bandarini atayakuta pale.

 

Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo akizungumza katika mkutano huo.

 

“Ndio maana kuna tofauti kati ya waandishi wa habari na watu wengine, niwapongeze kwenye suala hili mmekuwa mkifuatilia na kupewa taarifa sahihi na pia mnapotoa taarifa sahihi mtafanya hata wawekezaji waweze kuja kuwekeza kwenye tasnia hii.

 

“Na andikeni,chapisheni habari zenu bila uoga wala hofu, tumieni utaalamu wenu kuchapisha habari zenye ukweli na serikali imedhamiria kufanya maboresho ya sheria za habari na iko tayari kushirikiana na wadau katika kusaidia kuwa na ubora zaidi.

Picha ya pamoja mgeni rasmi na baadhi ya viongozi wa vyama vya waandishi wa habari.

 

“Najua mnapitia changamoto nyingi ikiwemo kutokuwa na vifaa vya kazi pamoja na maslahi lakini serikali kupitia Rais wetu, Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na waziri wetu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wamesema wapo pamoja na nyinyi na tutaangalia namna ya kufanya ili kuweza kutatua changamoto hizo.

 

“Waandishi wa habari wanawake wamepungua nchini kutokana na changamoto ya kukata tamaa kutokana na mazingira magumu ya kazi, hivyo hivi karibuni tutakaa kikao kupitia UTPC na kufanya kila liwezekanalo ili tuweze kutatua changamoto hizo” amesema Msigwa.

 

Naye rais wa UTPC Deogratius Nsokolo,amesema kuwa wana jumla ya vilabu 28 ambavyo 26 vipo Tanzania Bara na 2, Tanzania visiwani hivyo anategemea kuwa na UTPC bora zaidi kwa miaka ijayo.

 

“Kumekuwa na changamoto nyingi katika vilabu ambavyo vinapelekea kurudisha nyuma maendeleo mfano hapa Dar es Salaam tulikuwa hatuji kabisa lakini kwa sasa kuna uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Samson Kamalamo tunaona hata idadi ya wanachama inaongezeka kwa hiyo niwaombe wanachama wampe ushirikiano mzuri katika majukumu ya chama ili kuweza kuwa bora.

 

“Tunataka kuhamisha makao makuu yaweze kuwa Dodoma, kwa sasa tupo Mwanza, ili tuweze kuwa karibu na wanachama na wadau pamoja na serikali kwa urahisi zaidi, “amesema.

Leave A Reply