The House of Favourite Newspapers

Wachezaji 30 wa Gofu Washiriki Michuano ya Uhuru Golf Tournament Kilombero

0

 

 

Katika kusherehekea miaka 61 ya Uhuru, Klabu ya Gofu ya Kiwanda cha Sukari Kilombero imeandaa mashindano ya mchezo huo, yaliyowakutanisha washiriki 30 kutoka sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam na Morogoro.

 

Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Kiwanda cha Sukari Kilombero, Fakihi Fadhili amesema lengo la mashindano hayo ilikuwa ni kuwaleta pamoja wachezaji wa mchezo huo kwa lengo la kushindana, kufurahi pamoja lakini pia kuwahamasisha watu wengi zaidi kuupenda mchezo huo ambao una wachezaji wachache nchini ukilinganisha na michezo mingine.

 

 

Akaongeza kuwa pia mashindano hayo yatawapa nafasi wachezaji na wadau wa mchezo huo kukutana na kufahamiana zaidi.

 

Nahodha wa Timu ya Gofu ya Kiwanda cha Sukari Kilombero, Pierre Redinger, kwa upande wake aliutumia ufunguzi wa mashindano hayo kuwaelimisha wachezaji wa mchezo huo kuhusu kanuni mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa kwenye mchezo huo, ya kwanza ikiwa ni kuhakikisha unafurahi unapokuwa unacheza mchezo huo.

 

Mashindano hayo, yamefanyika katika Viwanja wa Gofu vya Kiwanda cha Sukari Kilombero chenye jumla ya mashimo 18.

 

 

 

Katika mahojiano, Morris Komba ambaye ni mchezaji mkongwe wa mchezo huo kutoka Klabu ya Gofu ya Kilombero, akatumia nafasi hiyo kuelezea machache kuhusu historia ya Klabu ya Gofu ya Kilombero na kueleza kwamba ilianzishwa mwaka 2002 na David Haworth ambaye kwa kipindi hicho ndiye aliyekuwa mkurugenzi wa kiwanda hicho, akishirikiana na Gerrie Odendaal ambaye alikuwa meneja wa kiwanda hicho kwa wakati huo.

 

 

Akaongeza kuwa kwa sasa klabu hiyo ina wachezaji 35 na kueleza kuwa klabu hiyo imekuwa ikishiriki kwenye mashindano mbalimbali kwenye mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Dar es Salaam na mikoa mingine.

 

Kwa upande wake, Vicky Elias ambaye ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Gofu, ameelezea kufurahishwa na mashindano hayo ambayo naye alikuwa miongoni mwa washiriki, na kuvisifia viwanja vya gofu vya Kilombero kuwa vina ubora unaoridhisha.

 

Akawataka wazazi kuwahamasisha watoto wao kushiriki kwenye mchezo huo, hususani watoto wa kike na kueleza kwamba kuna uhitaji mkubwa wa kuwaandaa wachezaji wapya wa mchezo huo ambao baadaye watajiunga na timu ya taifa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa na kuongeza kwamba amekuwa akifanya kazi ya kuwafundisha wachezaji wapya wa mchezo huo..

 

Dickson Sika, Katibu wa Chama cha Gofu cha Tanzania (TGU) ambaye naye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano hayo, naye akaeleza kufurahishwa na mashindano hayo, ikiwa ni mara yake ya pili kucheza kwenye viwanja vya Kilombero na kueleza kwamba wasichokijua wengi ni kwamba mchezo wa gofu ulitumika sana kipindi cha harakati za kupigania uhuru kuwaunganisha pamoja wanaharakati wote.

 

 

 

Leave A Reply