The House of Favourite Newspapers

Wachezaji Simba, Yanga Watoleana Vitisho vya Kibabe

0

KUELEKEA mchezo wa Simba dhidi ya Yanga mnamo Januari 4, mwakani, kumekuwa na tambo nyingi kutoka pande zote.

 

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa ukiwa ni raundi ya kwanza msimu huu, umekuwa na kawaida ya kuteka hisia za mashabiki wengi na hata wachezaji.

 

Hawa hapa baadhi ya wachezaji wa pande zote mbili waliozungumza na gazeti hili na kutoa tambo huku kila upande ukijinadi kuibuka na ushindi:

Dilunga: Tunawasubiri Yanga tu

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Hassan Dilunga ‘HD’ amefunguka kuwa wamejipanga kushinda mechi zote ikiwemo dhidi ya Yanga kwa kuwa malengo yao ni kutwaa ubingwa na sasa wanausubiria mchezo huo tu.

 

“Unajua malengo ni kuona kila mechi mbele yetu tunapata matokeo ya ushindi kwa sababu hatuhitaji kudharau wapinzani ambao wapo mbele yetu kwa kuwa tunachokiangalia ni kuweza kushinda kwa kila mechi,” alisema Dilunga.

Wachezaji wa timu ya Yanga.

Sibomana awachimba mkwara Simba

Mshambuliaji wa Yanga, Patrick Sibomana, amewaonya Simba kuwa wasitarajie mteremko kutoka kwao kama wanavyofikiria.

 

Sibomana, raia wa Rwanda, ametoa kauli hiyo licha ya Yanga kuwa kwenye nafasi ya nane ikiwa na pointi 18 tofauti na Simba inayoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 10.

 

“Unajua hii siyo ya kuichukulia kawaida kwa sababu  ya upinzani wa jadi ambao upo lakini kwangu naona ni mechi ngumu kwa sababu inakutanisha timu zenye historia kubwa ya soka la hapa, wapinzani wetu wanapaswa kujua kwamba tunahitaji matokeo mazuri ili kuweza kufikia ubingwa.

“Kiukweli tumejipanga vizuri kuona hatupotezi mchezo huo kwa hali yoyote kutokana na mabadiliko yanayoendelea kufanywa kwenye kikosi chetu, wanapaswa kujua kwamba sisi tunataka ushindi kutoka kwao ili kufikia malengo,” alisema Sibomana.

 

Ngassa:Tunawasubiri Simba bila presha

Mrisho Ngassa, kiungo mshambuliaji wa Yanga amesema kuwa kwa sasa wanaendelea na maandalizi yao ya mechi zao huku wakiipigia pia hesabu Simba kwa mbali.

 

“Ukitazama kwenye kalenda kila mechi imepangwa kwa utaratibu wake nasi tunahitaji pointi tatu, kwa mchezo dhidi ya Simba kwetu naona haupo mwanzo upo mbele hivyo lazima tupambane na hii iliyopo.

 

“Kikubwa ni kwamba hatuna mashaka na mchezo wowote wa ligi kwani tunahitaji pointi tatu na tutapambana kufanya vizuri, mashabiki watupe sapoti,” alisema Ngassa.

Ibrahim Mussa na Lunyamadzo Mlyuka

Leave A Reply