The House of Favourite Newspapers

Wafanyabiashara Shinyanga Wagoma

Wafanyabiashara wa soko la Nguzo nane mjini Shinyanga, wamegoma kuuza bidhaa zao kwa madai ya kuonewa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, kwa kuwatoza faini za mara kwa mara Shilingi 50,000 pamoja na kupewa risiti zilizoandikwa mwaka (2010), na kudai kuwa ni feki na huenda pesa zao zinaliwa.

 

Tukio la mgomo huo uliodumu kwa takribani saa tatu, limetokea leo Jumapili Novemba 25,2018 majira ya saa tatu asubuhi mara baada ya mkuu huyo wa wilaya kupita kwenye soko hilo, na kukuta baadhi ya bidhaa zikiwa chini na kumuita afisa afya wa manispaa hiyo Kuchibamba Kizito, ili kuwapiga faini wafanyabiashara wanne ambao wamekiuka maagizo na kuweka bidhaa hizo chini.

 

Akizungumzia mgomo huo katibu wa soko hilo Aidali Rashidi (Chinga) ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara waliotakiwa kupigwa faini Shilingi 50,000, alisema wamechoka na uonevu wa mkuu huyo wa wilaya, ambapo kila siku amekuwa akipita sokoni hapo na kuwapiga faini wafanyabiashara hao.

 

“Mkuu huyu wa wilaya mpya aliyekuja hivi sasa tumemchoka, amekuwa kila siku akipita hapa na afisa wake afya na kutupiga faini Shilingi 50,000 kwa wafanyabiashara wale ambao anakuta bidhaa zao zikiwa chini kwa aijli ya kuzipanga kwenye meza, na hataki maelezo yeye anacho angalia ni pesa tu,”alisema Rashidi.

 

“Leo asubuhi kama kawaida yake kapita hapa sokoni kakuta wafanyabiashara wakiwa wameweka bidhaa zao chini kwa ajili ya kuzipanga kwenye meza, akamwita afisa afya ili atupige faini na mimi nikiwamo, kitendo ambacho tumeona ni uonevu hivyo tukaamua kugoma kufungua biashara,”aliongeza.

 

Naye Ofisa afya wa manispaa hiyo ya Shinyanga Kuchibamba Kizito, alikiri kupewa maagizo na mkuu huyo wa wilaya kuwapiga faini Shilingi 50,000 wafanyabiashara ambao kila siku wanakutwa bidhaa zao zikiwa chini, na kutolea ufafanuzi suala la risiti kuandikwa (2010), kuwa ni kujisahau kuweka setting ya mashine.

 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ambaye alitoweka eneo la tukio, alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi na alisema suala hilo kwa sasa hawezi kulizungumzia, bali kesho ndiyo atafanya kikao na viongozi wote wa masoko mjini humo ili kuwekana sawa.

 

Aidha diwani wa Kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga Mahali lilipo soko hilo Hassani Mwendapole, aliutatua mgomo huo mara baada ya kufanya mawasiliano na mkuu huyo wa wilaya na Ofisa afya, na kuafikiana wafanyabiashara hao wafungue biashara zao na kutopigwa faini, bali wapewe kwanza elimu ya usafi.

Comments are closed.