The House of Favourite Newspapers

Wafaransa Wapiga Kura Katika Duru ya Pili ya Urais Kati ya Macron na Marine Le Pen

0
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akipiga kura yake na pembeni mwake ni mkewe Brigitte Macron.

Raia wa Ufaransa leo Jumapili Aprili 24, 2022 wamepiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Rais aliye madarakani Emmanuel Macron anachuana na Marine Le Pen kiongozi anayeelemea siasa za mrengo mkali wa kulia.

Uchaguzi huo wa rais nchini Ufaransa bila shaka utakuwa na athari zake katika mustakabali wa bara la Ulaya. Rais Emmanuel Macron ana kibarua kigumu katika pambano hilo dhidi ya mpinzani anayeelemea mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen.

 

Macron anayeelemea siasa za mrengo wa kati anawataka wapiga kura wamchague kwa kipindi kingine cha miaka mitano licha ya utawala wake kuakabiliwa na mfululizo wa maandamano ya kumpinga, janga la corona na vita katika Ukraine. Hata hivyi iwapo Macron ataibuka mshindi basi atakuwa rais wa kwanza wa Ufaransa katika kipindi cha miaka 20 kushinda muhula wa pili.

Mgombea wa urais wa Ufaransa Marine Le Pen akitoka kupiga kura yake.

Wakati huo huo matokeo kura ya nchini Ufaransa, taifa lenye silaha za nyuklia na moja ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani, yanaweza pia kuleta athari katika mzozo wa nchini Ukraine, wakati ambapo Ufaransa imekuwa na jukumu muhimu katika juhudi za kidiplomasia na pia ikiwa ni nchi iliyounga mkono vikwazo dhidi ya Urusi chini ya utawala wa Emmanuel Macron.

 

Kwa upande wake mpinzani wa Macron, bi Marine Le Pen umaarufu wake umeongezeka miongoni mwa wapiga kura wa Ufaransa. Kura za maoni zinaonyesha anamkimbiza Macron kwa kasi kuliko hapo awali.

 

Hata hivyo wengi wa wapiga kura wanaotarajiwa kumchagua Macron wanafanya hivyo ili kumzuia Le Pen kuyaendeleza mawazo yake yanayoonekana kuwa yanalemea mrengo mkali wa kulia na yanakiuka demokrasia, kama vile mpango wake wa kutaka kupiga marufuku kuvaa hijabu hadharani kwa wanawake wa Waislamu, au kutokana na uhusiano wake na Urusi.

Baadhi ya wapiga kura nchini Ufaransa.

Wagombea wote wawili katika kinyanga’anyiro hicho cha urais nchini Ufaransa wanajaribu kuzinasa kura zipatazo milioni 7.7 za wafuasi wa mgombea wa mrengo wa kushoto Jean-Luc Melenchon, aliyeshindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzim uliofanyika mnamo Aprili 10.

 

Kura zote za maoni katika siku za hivi karibuni zimetabiri ushindi kuelekea kwa rais Macron mwenye umri wa miaka 44 anayeunga mkono mshikamano wa bara la Ulaya ingawa tofauti ya kura kati yake na mpinzani wake wa mrengo mkali wa kulia Le Pen mwenye umri wa miaka 53 inaonekana wazi. Kwa sababu kura za maoni pia zinatabiri uwezekano wa idadi kubwa ya wapiga kura ambao watapiga kura zao lakini bila kuashiria waliomchagua au hata kutokupiga kura kabisa.

Leave A Reply