The House of Favourite Newspapers

Marekani: Wafuasi wa Trump Wavamia Bunge, Wanne Wauawa

0

WATU wanne wamefariki dunia akiwemo mwanamke mmoja aliyepigwa risasi kufuatia vurugu zilizoibuka baada ya wafuasi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuvamia bunge la nchi hiyo lililopo Capitol Hill na kupambana na polisi jana, Jumatano, Januari 6, 2020

Wafuasi wa Trump waliokuwa na hasira waliandamana huku wakiimba, “Tunamtaka Trump” huku mmoja wao akipigwa picha akiwa ameketi kwenye kiti cha rais wa bunge la Seneti. Vurugu hizo zimedumu kwa saa kadhaa kabla ya vikosi vya usalama kunusuru hali hiyo. 

Polisi jijini Washington imesema kuwa ni wazi waandamanji hao walikuwa tayari kutumia nguvu yoyote ile kuingia katika majengo ya bunge ambapo watu watu 13 wamekamatwa na silaha tano zimenaswa na polisi wakati ghasia zikiendelea bungeni. Mkuu wa Polisi, Robert Contee, amewaambia wanahabari kuwa waliokamatwa siyo wakazi wa eneo la Washington DC.

Rais Trump alilazimika kurekodi ujumbe kwenye video na kuutuma katika mtandao wa Twitter akitoa wito kwa wafuasi wake kuondoka katika majengo ya bunge lakini naye akawa anaendelea madai yasiyokuwa na ushahidi wowote kuwa Democrats waliiba kura.

Kumekuwa na na ishara kidogo zinazoonesha kwamba waandamanaji hao wanatii wito wa Rais Trump unaowataka warejee nyumbani licha ya kwamba mji huo wote unatekeleza hatua ya kutoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi.

“Najua machungu yenu, najua mumevunjika moyo…. Lakini lazima sasa murejee nyumbani, lazima tuwe na amani … hatutaki yeyote ajeruhiwe,” alisema Trump.

Mshindi wa urais wa nchi hiyo kutoka Chama cha Demokratic, Joe Biden, kwa upande wake amesema maandamano hayo “yamesababishwa na uchochezi na ni lazima hilo likome sasa“, amesema.

Kikao cha pamoja cha bunge kuidhinisha ushindi wa Biden kimeahirishwa na bunge limelazimika kwenda mapumzikoni. Kuna taarifa kuwa watu walitumia bunduki kwenye jengo hilo. Pia mabomu ya kutoa machozi yametumika kutawanya waandamanaji.

Wanajeshi na maofisa wa polisi pia wamepelekwa katika majimbo jirani huku maafisa wa Shirika la Ujasusi FBI wakipelekwa katika majengo ya bunge kusaidiana na maafisa wa polisi.

Wafuasi wa Donald Trump wenye hasira wamevuka mipaka ya usalama iliyowekwa na kusimama kandokando ya bunge huko Washington, wakati wabunge wanakutana kumuidhinisha rais mteule Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.

Katika matukio ya kutatanisha, waandamanaji walizunguka jengo la bunge huku wabunge nao wakisindikizwa kutoka bungeni humo na polisi. Pia, amethbitisha kuwa baadhi ya maafisa wanapata matibabu baada ya kujeruhiwa.

Waandamanaji walikuwa wanalenga nini?

Kikao maalum cha bunge kilikuwa kinaendelea kuidhinisha ushindi wa Biden katika uchaguzi wa Novemba 3. Kawaida vikao kama hivyo huwa vinachukua muda mfupi sana na vyenye kufurahiwa lakini wabunge wa Republican wamekuwa wakipinga baadhi ya matokeo ya uchaguzi.

Kwa siku kadhaa sasa Trump amekuwa akimshinikiza Pence, ambaye anaongoza kikao hicho, kuzuia uidhinishaji wa matokeo hayo. Lakini katika barua iliyoandikiwa bunge Jumatano, Pence alisema hana “mamlaka ya moja kwa moja ya kuamua ni kura gani za wajumbe zitahesabiwa”.

Waandamanaji walifika katika majengo ya bunge kutoka kwa mkutano uliopewa jina la “Save America Rally”, ambapo Bwana Trump aliwataka wafuasi wake kuunga mkono wabunge wanaopinga kuidhinishwa kwa Biden kama mshindi.

Trump alikataa ukubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi wa Novemba 3 na kudai mara kadhaa kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote. Jumatano Trump alisema tena: “Hatutachoka. Hatutakubali kuwa tumeshindwa.”

Pia, ameonesha kutilia shaka uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumanne katika jimbo la Georgia. Katika ubashiri wa jinsi matokeo yalivyo kwenye uchaguzi huo wa marudio kulingana na vyombo vya habari vya Marekani, inaonekana chama cha Democrats kimeshinda kiti kimoja huku washindani wakikaribiana mno katika kiti kilichosalia.

Ikiwa Democrats itashinda viti vyote, Bwana Biden atakuwa na udhibiti wa bunge la Seneti na hilo litasaidia kupitisha ajenda zake baada ya kuapishwa rasmi kama rais wa Marekani Januari 20.

Viongozi Duniani Walaani Uvamizi wa Bunge Marekani

Kitendo hicho kimelazimisha kuahirishwa kwa muda kikao maalum cha kumuidhinisha Biden mshindi. Viongozi wengi wametoa wito wa amani na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya utulivu, wakielezea uvamizi uliotokea kama wenye “kuogofya na uvamizi wa demokrasia”.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amelaani kitendo hicho na kusema ni “aibu”…. “Marekani inasimamia demokrasia kote duniani na ni muhimu sana kuwa na ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani na wenye mpangilio,” ameandika kwenye mtandao wa Twitter.

Viongozi wengine wa kisiasa Marekani wamekosoa ghasia hizo huku kiongozi wa upinzani Sir Keir Starmer akitaja kitendo hicho kama “uvamizi wa moja kwa moja wa demokrasia”.

Waziri wa kwanza wa Scotland, Nicola Sturgeon, ameandika kuwa kinachotokea bungeni “kinatia hofu mno”. Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, amesema: “Nina imani na demokrasia ya Marekani. Uongozi wa rais mpya Joe Biden utakabiliana na kipindi hiki kigumu, kuunganisha watu wa Marekani.”

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amelaani kitendo hicho na kusema ni “uvamizi mbaya dhidi ya demokrasia”, huku mwenzake wa Ujerumani, Heiko Maas, akisema bwana Trump na wafuasi wake “lazima wakubali uamuzi wa wapiga kura wa Marekani na waache kutatiza demokrasia”.

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, amesema kuwa aliamini sana Marekani “katika kuhakikisha ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani” kwa Bwana Biden, na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema ana matarajio makubwa ya ushirikiano na chama cha Democrat.

Katibu Mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg, aliungana na wale waliosema matokeo ya uchaguzi ni lazima yaheshimiwe. Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, amesema raia wake “wamehuzunishwa sana na kitendo hicho cha uvamizi wa demokrasia”.

Leave A Reply