The House of Favourite Newspapers

Wafugaji, wakulima wachomana mikuki!

0

wakulima na wafugaji (1)

Ramadhan Botea aliyejeruhiwa mkononi.

Richard Bukos na Issa Mnaly, Uwazi

PWANI: Hali si shwari katika Kijiji cha Geza Ulole, Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Pwani kufuatia wafugaji wa Kimang’ati na wakulima kuwindana usiku kucha na kuchomana mikuki kisa kikitajwa kuwa ni migogoro ya malisho ya mifugo, Uwazi lilifuatilia.

Chanzo kilidai kuwa hali hiyo imewafanya wakulima kushindwa kwenda mashambani kwa kuwa mifugo inaposhambulia mazao yao na wanapojaribu kuiondoa, ndipo mapigano huanza.

Kufuatia hali hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili  lilikwenda kwenye kijiji hicho kujionea hali halisi ambapo lilishuhudia baadhi ya mazao yakiwa yameharibiwa huku baadhi ya wakulima wakiwa wamejeruhiwa.

Mashaka Mrisho (55), mkazi wa kijiji hicho ambaye  alichomwa mkuki mgongoni na kutokea tumboni kufuatia mapigano yaliyotokea Mei, mwaka huu, alikuwa na haya ya kueleza:

wakulima na wafugaji (5)Wanakijiji wakihojiwa na Uwazi.

“Nakumbuka mwezi mmoja uliopita, saa sita usiku, nikiwa nimelala, nilisikia kelele za kuomba msaada kwenye nyumba ya jirani yangu, Athuman Adam. Nilitoka kumsaidia, kumbe alikuwa akishambuliwa baada ya kuvamiwa na wafugaji hao.

“Nilipofika nilimkuta Athuman ameshacharangwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na kupigwa rungu la kichwa lililomfanya azimie.

“Nikiwa kwenye juhudi za kutaka kumuokoa, waliingia tena na kuanza kunishambulia kwa sime na marungu kisha kunichoma mkuki mgongoni ambao ulitokea mbele kwenye kitovu.

wakulima na wafugaji (3)Mashaka Mrisho aliyechomwa mkuki.

“Nilipoteza fahamu na nilipozinduka, nilijikuta nipo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Dar) nikipatiwa matibabu.

“Nikiwa Muhimbili walionifanyia unyama huo walibainika na kufunguliwa kesi ya shambulio la kudhuru mwili yenye jalada namba BAG/RB/1417/2016 lakini nikasikia wameachiwa kabla sijatoka hospitali.

“Hivi mnavyoniona wameshanipa ulemavu, siwezi tena kufanya kazi ngumu kama nilizokuwa nikifanya awali na kuilea familia yangu,” alisema mkazi huyo.

wakulima na wafugaji (2)Mashaka Mrisho akionesha jeraha mgongoni

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Ramadhan Botea (62) alisema siku ya tukio, saa nane mchana akiwa shambani kwake, mfugaji aliyemtambua kwa jina la Meugu, alivamia kwenye shamba lake na kuingiza mifugo iliyoanza kula mazao.

“Nilipoona mifugo ikishambulia mazao yangu, roho iliniuma sana kwani nilikuwa nategemea mazao hayo kuendesha maisha yangu.

wakulima na wafugaji (4)

“Nilijaribu kuizuia ndipo yeye na kijana aliyekuwa naye walianza kunishambulia kwa sime na marungu. Ukweli na uzee huu walinidhalilisha sana maana nilianza kulia kama mtoto lakini waliendelea kunicharanga na sime na kunipiga marungu na fimbo kama mwizi.

“Wakati huo, mwanangu na mke wangu walikuwa wakiniangalia ninavyodhalilishwa lakini hawakuweza kupambana nao. Hata hivyo, iliwauma sana,” alisema mzee Botea akionesha majeraha na mkono wa kulia aliofungwa plasta ngumu P.O.P.

Wakiendelea kutoa kilio chao, Shukuru Ramadhan alisema wiki mbili zilizopita, saa saba usiku, wafugaji hao walivamia nyumba yao kwani walisikia mbwa akibweka, ndipo mumewe aliyemtaja kwa jina la Manjebe Katikiro akatoka kupambana nao.

Wafugaji hao walimkamata na kumshambulia kwa kumkata sime na kumpiga marungu kichwani kisha kubomoa zizi lenye ng’ombe wanne waliokuwemo na kuwaiba.

“Kitendo hicho kilimpa hasira mume wangu, asubuhi baada ya kupata fahamu aliingia msituni kuwasaka na hajarudi tangu siku hiyo, sijui kama yuko hai au la,” alisema mwanamke huyo.

Baadhi ya wanakijiji wengine walioshambuliwa na kuharibiwa mazao yao ni Daudi Juma, Emmanuel Erasto na Cecilia Daudi (picha namba 1 Uk. 3), Mariam Shirinde ( picha namba 2 Uk. 3)

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Geza Ulole Kata ya Makurunge, Tabu Luaga alikiri kutokea machafuko hayo kwenye kijiji hicho na kusema wafugaji hao walishapewa amri ya kuhama lakini bado wanaishi kwa ukaidi.

“Hawa wafugaji walishahamishwa  eneo hili tangu yalipoanza machafuko lakini wanaonekana kukaidi agizo la serikali, kinachotakiwa ni jeshi la polisi kutumia nguvu,” alisema mwanamke huyo.

Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Bagamoyo, Adam Maro alipotafutwa, alisema anazo taarifa za matukio hayo lakini akawalaumu viongozi wa vijiji kwa kuchelewa kumpelekea taarifa wanapoona makundi ya ng’ombe na wachungaji wasiowaelewa kwenye vijiji vyao.

Alisema migogoro hiyo imekuwa sugu lakini wao kama jeshi la polisi, hawahusiki kuitatua bali wanaingia pale panapotokea machafuko.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bonaventure Mshongi kuzungumzia sakata hilo, simu yake haikupatikana hewani.

Kwa mahojiano zaidi kuhusu sakata hili, usikose kutazama Global TV Online kwa kubofya www.globaltvtz.com.

Leave A Reply