The House of Favourite Newspapers

Wafungwa 136 Waachiwa Huru Simiyu, Kicheko Kama Chote

0

JUMLA ya wafungwa 136 kutoka magereza ya Mkoa wa Simiyu wamechiwa huru kufuatia msamaha wa RaisJohn Pombe Magufuli alioutoa Desemba, 2019 katika sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza.

 

Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari Desemba 10, 2019 Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Simiyu, ACP. Andulile Mwasampeta amesema anamshukuru Mheshimiwa Rais Magufuli kwa msamaha huo  ambao umesaidia kupunguza msongamano kwenye magereza ya mkoa huo.

“Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kutoa msamaha huu ambao umepunguza msongamano katika magereza yetu hususani gereza la Bariadi.  Nitumie nafasi hii kuwaasa wafungwa waliosamehewa kwenda kuwa raia wema na wakafanye kazi halali na wasifanye makosa yatakayowaleta tena hapa gerezani,” alisema.

 

Aliongeza  kuwa wafungwa 136 waliopata msamaha huo katika mkoa wa Simiyu ni wale waliokuwa wamebakisha muda wa siku moja hadi miezi sita na miezi 12 kumaliza muda wa vifungo vyao, ambapo amebainisha kuwa wamezingatia maelekezo ya rais katika vigezo vya watu walioachiwa huru.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka,  kwa kufanikisha zoezi la kuwaleta pamoja wafungwa wote waliopata msamaha huo, alitoa magari yaliyowezesha jeshi la magereza kuwachukua katika magereza mbalimbali mkoani Simiyu na kuwaleta katika gereza la Bariadi ambapo ndipo walipoanzia safari ya kurejea majumbani kwao.

 

Kwa upande wao wafungwa waliopata msamaha huo wamemshukuru Rais Magufuli  na kuahidi kuwa raia wema watakaofanya kazi halali na kujiepusha na makosa yote yanayoweza kusababisha wakarudi tena gerezani.

 

“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa msamaha huu alioutoa kwa wafungwa zaidi ya 5,000 tuliokuwa katika magereza mbalimbali.  Niseme tu kwamba wale wote waliokuwa wafungwa kama mimi na wakapata msamaha huu tukawe raia wema na tukachape kazi tujenge nchi yetu, “ alisema Buluba George miongoni mwa wafungwa 136 mkoani Simiyu.

 

“Mimi naahidi kwenda kujishughulisha na kazi za kuniwezesha kupata kipato, nitajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili nisije nikaletwa tena huku gerezani, namshukuru sana Rais Magufuli kwa kutupa msamaha huu,” alisema Musa Lazaro miongoni mwa wafungwa 136 mkoani Simiyu.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Leave A Reply