The House of Favourite Newspapers

Wahindi Wekundu; Wanaotembea Bila Nguo, Walaji Wa Nyani!-3

0

KATIKA mfululizo wa makala za safu hii, naendelea kukuletea Wahindi Wekundu wa Kabila la Huarorani, hawa wanaishi kwenye misitu ya Amazoni huko Jamhuri ya Ecuador.

Niliandika kuwa nchi hii ipo Kaskazini Mashariki ya Bara la Amerika ya Kusini na inapakana na nchi ya Colombia iliyo Kaskazini mwa nchi hiyo na kwa upande wa Mashariki inapakana na Bahari ya Pasifiki.

Kabila tunaloendelea kulijadili leo ni la watu wanaoitwa Wahuaorani, Waorani au Waodani, lakini watu wengine kutokana na urefu wa jina hilo wanaita Waos, wanaoishi katika Mkoa wa Amazon.

Watu hawa wana tabia za ajabu tofauti na jamii nyingine duniani. Kwanza ni ile tabia ya kutovaa nguo kabisa.

Kuna wakati kunakuwa na sherehe maalum kwa wanawake na wanaume, ni maalum kwa waliovunja ungo kwa wanawake na waliobalehe kwa wanaume.

Katika shehere yao, kama mtu aliyestaarabika atahudhuria atashangazwa kwani atashuhudia ajabu kubwa kwa kuona wanaume, wanawake, vijana wa kike na kiume na watoto, wote wakiwa hawana nguo na wanafanya sherehe zao bila wasiwasi wowote.

Wasichana waliovunja ungo huwekwa ndani kwenye nyumba za nyasi kwa siku kadhaa kwa ajili ya kupewa mafunzo maalum ya utu uzima.

Siku ya kutoka, huandaliwa sherehe ambapo husimamishwa kwenye foleni wakiwa uchi na kupita mbele ya umati huku kichwani wakiwa wamevikwa manyoya ya ndege yaliyosuka kwa ustadi mkubwa.

Kwenye sherehe hiyo huandaliwa nyama ya nyani au nguruwe ambayo imebanikwa huku wazee wakiandaliwa pombe maalum na wasichana wanaopita mbele ya wazee hao, huinama, ishara ya kutoa heshima kisha hulipuka kelele za kuwashangilia.

Kama tulivyoona katika toleo lililopita, nyama hizo za nyani na nguruwe hupatikana kwenye misitu na ni kazi ya kuwinda hufanywa na wanaume na nyama hiyo ya sherehe hutafutwa na vijana waliobalehe mwaka huo baada ya vijana hao kufundishwa jinsi ya kuwinda, kama kazi ya kuitegemea maishani.

Wakiwa porini hufundishwa jinsi ya kutumia silaha za jadi ambazo ni upinde na mishale pamoja na mikuki kuua wanyamapori.

Wahuaorani huwafundisha pia vijana wa kiume waliobalehe jinsi ya kutumia mitego ya kienyeji kunasa wanyama wanaowataka maporini.

Kwa kuwa wakati wa sherehe maalum nyama hutumika sana hasa ya nyani ambayo wanaitaja kuwa ni tamu sana kuliko nyama nyingine, wavulana hupewa jukumu la kuua nyani wengi wa sherehe. Wanyama hao huwindwa kwa kutumia pia mishale maalum midogo ya kupuliza, kwamba nyani wanapoona watu, hukimbilia juu ya miti na watu hao huwa na vijiti maalum ambavyo huwa wamevipaka sumu na kuwapulizia.

Vijiti hivyo ambavyo huwekwa kwenye mwanzi maalum humpata nyani na kumchoma, hivyo ile sumu kumuingia mnyama huyo na kufa.

Fuatilia simulizi hii ya kweli uone maajabu ya dunia Jumanne ijayo hapahapa!

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO

Leave A Reply