The House of Favourite Newspapers

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi Wachangia Milioni 30 Ujenzi wa Msikiti

0
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi mchango wa shilingi milioni 30 zilizotolewa na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na usalama kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 27, 2020.

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamekabidhi Shilingi milioni 30  ujenzi wa msikiti wa kisasa wa  Wilaya ya Chamwino Mkoani  Dodoma.

 

Akikabidhi mchango huo leo Agosti 27, 2020 kwa niaba ya wakuu wengine wa vyombo hivyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa wameguswa na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwawezesha wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo ya imani .

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akimkabidhi Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge mchango wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma unaojengwa na SUMA JKT ambaye ni mkandarasi wa mradi huo.

“Naamini kuwa michango zaidi itaendelea kutolewa ili azma ya kujenga msikiti huu ikamilike kwa wakati”, Alisisitiza Jenerali Mabeyo

 

Hafla ya Kukabidhi fedha hizo imefanyika pembezoni mwa msikiti wa zamani unapojengwa msikiti huo mpya ambapo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Venance Mabeyo amekabidhi fedha hizo kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali, Charles Mbuge, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, inayotekeleza mradi huo.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza wakati wa hafla ya kupokea mchango wa Wakuu Vyombo vya Ulinzi na Usalama waliochangia milioni 30 na Wakuu wa Mikoa ambao wamechangia shilingi Milioni 26 katika ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 27, 2020.Mkandarasi wa mradi huo ni SUMA JKT.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa  kiasi cha Shilingi milioni 142 zimeshachangwa na wadau mbalimbali ili kuwezesha ujenzi wa msikiti huo.

Alipongeza jitihada za kuwafanya watanzania kushikamana bila kujali imani zao kutokana na ushirikiano ulioneshwa na wadau mbalimbali katika kuchangia ujenzi wa msikiti huo.

 

Kwa upande  wa Wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara,nao pia wamekabidhi shilingi milioni 26 kwaajili ya Ujenzi huo.

Sehemu ya Wakuu wa Mikoa walishiriki katika hafla hiyo wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo kabla hajakabidhi mchango wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwezesha ujenzi wa Msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Mikoa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evaristi Ndikilo amesema kuwa wanaunga mkono juhudi za ujenzi wa msikiti huo zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

 

Aidha, Pamoja na Fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka,amekabidhi shilingi milioni mbili zilizochangwa na kanisa la AICC la mkoani humo.

 

Kwa upande wake, Sheikh mkuu wa Wilaya ya Chamwino Suleiman Matitu  amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuchangia ujenzi wa msikiti huo na kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia.

Shehe wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Bw. Suleiman Matitu akitoa neno la shukrani kwa Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Mikoa waliochangia katika ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino.

Aidha, Shehe Matitu aliwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na  Wakuu wa mikoa  kwa kuchangia ujenzi wa msikiti huo.

Azma ya kujenga msikiti mpya wa Wilaya ya Chamwino ilianzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni wakati wa ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki  la Mt. Immaculata Chamwino ambapo alizindua kanisa hilo  baada ya kuchangia ujenzi wake na ukarabati.

Katika kuendeleza azma hiyo alianzisha  harambee ya ujenzi wa msikiti huo ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi Milioni 142 zimeshapatikana.

 

Ujenzi wa Msikiti huo unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT na tayari vifaa na malighafi mbambali zimeanza kufikishwa  katika eneo la ujenzi ili kazi ya ujenzi iweze kuanza mara moja.

Leave A Reply