The House of Favourite Newspapers

WALIOFARIKI AJALI YA MV NYERERE WASIMULIA AJALI ILIVYOTOKEA!

NI usiku mnene. Nipo juu ya kilele cha mlima. Nasikia kelele za wanyama, nasikia baridi kali sana. Nikaanza kushuka chini ya mlima ili angalau nikajistiri na baridi hiyo. Wakati nakaribia kufika chini ya mlima huo, nikaanza kusikia biti ya muziki fulani wa Bongo Fleva…

 

Aaaah dunia aaaaah…

Bado ni kiza na marashi ya dunia siyasikii, najihisi niko kuzimu naishangaa sayari hii. Iliyojawa wanasiasa michezo na wasanii, najiuliza umekuja huku kutalii au wameshamia dunia ndio haijirudii, mara nasikia swali kama la nguvu za hoja, Dandu ananiuliza albamu zinajikongoja, vipi mmegonga kopi chini ya milioni moja, jibu zinalipa siyo moja kwa moja, Steve 2K anauliza bifu zinaendelea, nimeshamsamehe Castro ameshatoka Segerea, namjibu bifu lipo na vita vinanyongea, Castro bado anaoza tuanzeni kumuombea, Complex naye anauliza albamu ile ya wagosi walishagonga kopi ngapi hadi sasa kwa wadosi, namjibu tangu ufe mambo yote ni mikosi, makundi yanavunjika duniani tunakumisi…

 

Eeeee eiiiihe ieeeeeee…

Nikagundua ni wimbo wa majonzi wa staa wa Bongo Fleva, Matonya. Ghafla wimbo ukazima. Giza likaondoka na nilichokiona mbele yangu ni watu takriban 224 ambao baada ya kuzungumza nao, nikatambua kuwa ni wale waliofariki katika ajali ya MV Nyerere, wakiwa na viongozi mbalimbali waliotangulia mbele za haki miaka mingi iliyopita.

 

Nilimuona Mwalimu Julius Nyerere, nikamuona Kapteni Komba, nikamuona Edward Sokoine. Mazungumzo yetu yalikuwa hivi:

Mmoja waliokuwa kwenye meli aliyejitambulisha kwa jina la Juma: Wewe mwanahabari vipi? Umefata nini huku?

Mimi: Hata sijui ilikuwaje lakini nimejikuta tu niko hapa na kusema ule ukweli ile ajali yenu imeacha simanzi kubwa sana…

 

Juma: Simanzi kubwa sana umeipimaje?

Mimi: Msiba ulitangazwa kuwa wa Kitaifa. Bendera ilipepea nusu mlingoti kwa siku nne. Halafu kwanini kwenye ajali yenu kila mtu alikuwa anaongea lake…

Juma: Kuhusu nini?

Mimi: Kwamba sijui kivuko kilibeba watu wengi kuliko uwezo wake, sijui kulikuwa na magari mengi, hivi mlikuwa wangapi kwani?

 

Juma: Wewe umeamini lipi?

Mimi: Kwa kweli nimebaki na lile la watu 265 ambalo alitangaza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele.

Juma: Nafikiri atakuwa hajakosea sana, tulikuwa tunacheza kwenye idadi hiyo…

Nyerere: Jamani mbona sijawaelewa? Ina maana kile kivuko kilichopewa jina langu kimezama kule Mwanza?

 

Mimi: Ndio, hujakosea mzee hapa acha niendelee kuzungumza nao, utapata picha kamili…

(Nikamuuliza Juma tena swali) Hivi siku ile ilikuwaje mkajaa wengi vile, nyinyi hamkuona kama ni hatari kwenu?

Juma: Sisi ni abiria wa kawaida, hatuna elimu ya kujua idadi halisi ya watu wanaohitajika kwenye kivuko hicho.

 

Mimi: Wakati kinaondoka hamkuona kama kinapata shida kutembea?

Juma: Hapana, kilienda vizuri na mpaka jirani yangu niliyekuwa nimekaa naye akaniambia leo kina spidi kweli, nafikiri ni baada ya kubadilishiwa injini hivi karibuni.

Mimi: Wakati ajali inatokea mlikuwa kwenye mazingira gani? (mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John akadakia…)

 

Tulikuwa tayari tumeshajiandaa kushuka maana ni jirani kabisa na eneo la kutia nanga…

Mimi: Aisee poleni sana…

John: Nionavyo mimi kuna uzembe mkubwa, hawakupaswa kutuacha tujae vile wakati wanajua uwezo wa kivuko hicho.

 

Mimi: Tayari Rais Dk John Pombe Magufuli ameshaivunja bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA), ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na pia imeundwa kamati maalum ya uchunguzi juu ya tukio hilo.

 

John: Ni sawa acha wafanye uchunguzi lakini kwa kweli kupitia tukio hili kama nchi inapaswa kujifunza, MV Victoria ilizama na sisi tumezama, vivuko, meli zote nchini zinapaswa kutazamwa upya. Kuwe na watu makini wa kusimamia, vinginevyo majanga ya aina hii hayawezi kuisha.

(Nyerere akadakia).

 

Nimekuwa nikisikia habari za rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli, mimi nimuombe tu awachukulie hatua kali wahusika na matukio ya aina hii yasitokee kizembe.

Mimi: Ni kweli, kwa yule tuna imani, hatopona mtu ambaye amehusika kwa namna yoyote ile.

Juma: Mazishi yetu yaliwaje?

 

Mimi: Mlizikwa kitaifa. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliongoza mazishi yenu, walikuwepo mawaziri, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Venance Mabeyo, mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella na mamia ya watu… Kwa kweli mimi nataka kuondoka huku jamani mbaki salama?

John: Uondoke kivipi? Hapa ndio tumefika…

Wakati natafakari kauli hiyo ya John, ghafla nilishtuka na kujikuta nipo kitandani kwangu kumbe nilikuwa naota!

SAA TISA USIKU KITANDANI KWANGU | NA ERICK EVARIST

 

Mzee wa Ukara: “Ukifa majini huvalishwi sanda” | Mke Analala na Mwanaume Mwingine

Comments are closed.