The House of Favourite Newspapers

WALIOMKERA JPM KORTINI

MBEYA: MAOFISA watatu waliomkera Rais Dk. John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake mkoani hapa hivi karibuni, wamefikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini hapa kutokana na tuhuma wanazotuhumiwa. 

 

Akisoma kesi ya jinai namba 01/2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mbeya, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sospiter Tyeah aliwataja washtakiwa kuwa ni Beliezery Malila (56) ambaye ni Afisa Ushirika Wilaya ya Kyela, Wilson Maneno Mwaisumo (79) aliyekuwa Meneja wa Chama cha Ushirika Kajunjumele na mshtakiwa wa tatu ni Nelbert Ikinga Mwakinyengela (60) ambaye alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Ushirika Kajunjumele.

 

Mwendesha mashitaka huyo alisema washtakiwa wote watatu wanashtakiwa kwa kosa la kula njama ya kutenda kosa, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 384, kosa wanalodaiwa kutenda kwa tarehe tofauti kati ya Machi 05 na Aprili 10, mwaka huu wilayani Kyela, mkoani Mbeya.

 

Alimtuhumu mshtakiwa wa kwanza kuhusika kwa kosa la kughushi nyaraka kwa nia ya kudanganya kwa kutumia muhuri unaoonesha kuwa ni kutoka ofisi ya Chama cha Ushirika Kyela huku akijua kuwa si kweli. Alisema kosa hilo ni kinyume na kifungu namba 333, 335 (A) na 337 sura ya 16 ya makosa ya jinai iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

 

Wakili huyo wa serikali alisema kosa la tatu ni kwa mshtakiwa wa pili na tatu ambalo ni kughushi muhtasari wa kikao cha bodi kisha kuziwasilisha nyaraka hizo kwa Meneja wa Benki ya NMB, Tawi la Kyela ambazo Takukuru inadai ni za uongo. Kosa la nne la kughushi, alisema ni kinyume na kifungu namba 342 na 347 sura ya 16 iliyorejewa mwaka 2002. Baada ya kusomewa tuhuma zao, washtakiwa wote walikana makosa hayo yote.

 

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo. Hata hivyo, washtakiwa hao wamerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi Mbeya, Venance Mlingi ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 20, mwaka huu kesi itakapotajwa.

 

Dhamana kwa washitakiwa ipo wazi, ambapo wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali au taasisi ya umma wakiwa na barua ya uthibitisho na bondi ya fedha shilingi 15 milioni kila mmoja na kuonywa kutosafiri nje ya mkoa bila kibali cha mahakama.

 

Hivi karibuni Rais Magufuli akiwa ziarani, wilayani Kyela, alimwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, kufanya uchunguzi suala la madai ya ubadhirifu katika chama cha ushirika wilayani humo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.

STORI: EZEKIEL KAMANGA, RISASI JUMAMOSI

Comments are closed.