The House of Favourite Newspapers

Wamerogwa ama?

0

Jux na Vee Money.

Andrew Carlos

PATA picha upo eneo tulivu, masikioni umeweka ‘headphones’ na unasikiliza nyimbo za wakali wa muziki Bongo, unaanza na nyimbo za Juma Musa ‘Jux’ kisha unafuatia za mkali wa Hip Hop, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’.Hamu inakuwa haijaisha vizuri kwa upande wa Hip Hop, unaamua kusikiliza nyimbo za Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’ kisha unachukuwa juisi na kumalizia fundo la mwisho.

Nikki wa Pili na Joh Makini.

Kabla hujainuka kuondoka eneo hilo, unaamua kusikiliza nyimbo za ‘pacha’ wa Bongo Fleva, Chegge na Temba lakini kuna kitu kinakupa hasira.Kwa nini ‘hawasongi’ kimataifa? Unavuta tena picha, Jux yupo karibu sana na Vanessa ‘Vee Money’, Diamond na Chegge na Temba, Mwana FA na AY, Nikki wa Pili na Joh Makini na wenzao wote wanatambulika kimataifa. Swali linakujia WAMEROGWA AMA?

Jux na Vee Money
Hakuna asiyekubali uwezo wa Jux katika muziki wa R&B nchini, mkali huyu anabamba kinoma na ngoma kama vile Sisikii, Nitasubiri, Uzuri Wako na nyingine nyingi. Amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Vee Money tangu mwaka 2014. Uhusiano wao ulifika mbali zaidi kwani walikuwa pamoja katika ‘tour’ mbalimbali ndani ya nchi.

Tangu mwaka huo 2014 hadi sasa Vee Money ameshashiriki katika tuzo za kimataifa zaidi ya tatu yaani All Africa Music Awards (Afrima), MTV Africa Music (MAMA) pamoja na African Muzik Magazine Awards (Afrimma). Mbali na tuzo hizo, Vee Money ameshapiga shoo kibao za kimataifa akiwa peke yake (Marekani, Afrika Kusini, Nigeria n.k) ambazo zimemfanya kujulikana kila kukicha na wanamuziki wa kimataifa. Kwa upande wa Jux, asilimia kubwa anajulikana ndani ya nchi tu. Hakuna dalili yoyote ya ‘kushikwa mkono’ kimataifa na Vee Money.

Nikki wa Pili na Joh Makini
Ni kati ya ndugu wanaokimbiza katika muziki wa Hip Hop Bongo. Mastaa hawa wanaunda kundi la Weusi wakiwa na wenzao G Nako pamoja na Bonta. Katika sherehe ya Zari All White iliyofanyika Mei mwaka huu, staa wa Hip Hop kutoka ‘Sauz’ AKA alikuwa mmoja wa waalikwa na ujio wake huu ulimfanya Joh Makini kupata nafasi ya kolabo naye.

bali na kufanikiwa kolabo hiyo, Joh ameshatoka na Ngoma ya Nusunusu ambayo kwa mara ya kwanza video yake ameifanyia nchini Afrika Kusini na hivi sasa yupo mbioni kutoka kimataifa zaidi na staa wa Nigeria, Davido. Juhudi zote hizo bado hazionekani ‘kumbeba’ Nikki wa Pili kumpeleka kimataifa.

Diamond vs Chegge na Temba

Haina mjadala kama Diamond kwa sasa ndiye mwanamuziki anayekubalika zaidi nchini Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika. Amekuwa akijizolea tuzo lukuki za kimataifa na hivi karibuni aliweka historia Ulaya kuwa Mtanzania wa kwanza kuchukua Tuzo ya MTV EMA akimpiku mwanamuziki na aliyewahi kuwa mrembo wa dunia 2000, Priyanka Chopra kutoka India.

Lakini nyuma ya pazia, wanaomuongoza Diamond kuelekea mafanikio yake ni haohao wanaowaongoza Chegge na Temba. Diamond amejizolea heshima kubwa nchini Nigeria na Sauz lakini juhudi za kuwapeleka kimataifa zaidi Chegge na Temba hazionekani. Mara ya mwisho pacha hao walifanikiwa kutinga Sauz na kufanya Ngoma ya Kaunyaka lakini bado haukuwafanya kubamba kimataifa na hii inaonekana sapoti kutoka kwa Diamond ipo chini.

Mwana FA vs AY
YUPO kimya lakini akiachia ngoma huwa gumzo kila kona, Ngoma yake ya mwisho ilikuwa Mfalme ambayo ilikuwa gumzo kutokana na mashairi na kumpelekea kuibuka na Tuzo za Kili 2015. Muda mrefu FA amekuwa ‘swahiba’ wa AY na kuna kipindi walijiunga pamoja kama kundi na kufanya muziki kisha kila mmoja akarudi kufanya muziki kivyake.

Mbali na kuwa karibu lakini hakuna dalili ya FA kushikwa mkono na AY kufanya muziki wa kimataifa. AY hadi sasa anashikilia tuzo nyingi za kimataifa kutoka Channel O, MTV Music (Mama) na ameshafanya shoo kibao za kimataifa sambamba na kufanya kolabo na mastaa wakubwa duniani kama vile Sean Kingston, Lil Romeo na wengine kibao. Pia AY ndiye balozi wa Godfather (kampuni kubwa ya Sauz inayowatengenezea mastaa video za kimataifa).

Leave A Reply