- Itarushwa Kimolita 400 angani hivi karibuni
- Itakuwa msaada mkubwa kwa wakulima
- Watafiti kuitumia kupata taarifa mbalimbali
WANAFUNZI na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha jijini Dar es Salaam, wamebuni Satellite ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu Dola za Marekani 250,000.
Wanafunzi hao ni Steven Makunga, David Seng’enge na Doris Ndaki wanaosoma Shahada ya Sayansi ya Kompyuta mwaka wa pili wakisaidiwa na mwalimu wao, Dk. Amani Bura.
Utengezaji wa Satellite hiyo umefikia asilimia 50 na inatarajiwa kurushwa angani kuanzia mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka 2024 kutoa taarifa mbalimbali.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliab Opiyo, alisema mradi huo wa Satellite unatekelezwa na wanafunzi na wahadhiri wa Kitivo cha Uhandisi na teknolojia chuoni hapo.
Alisema wanatarajia kuipeleka Satellite hiyo aina ya 3U Cubesat Kilomita 400 angani kuwezesha ukusanyaji wa taarifa kwaajili ya tafiti kwenye maeneo mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabia nchi na mienendo ya wanyamapori.
Profesa Eliab alisema walianzisha mradi huo miaka miwili iliyopita na kwamba kazi inayofanyika kwa sasa ni kutengeneza mfano wa Satellite na kuifanyia majaribio kadhaa na kuongeza kuwa walishaionyesha kwenye maonyesho ya MAKISATU mkoani Dodoma.
Alisema watakapoirusha angani itawasaidia kupata taarifa mbalimbali kwa taasisi na watafiti wanaotafuta taarifa mbalimbali.
Alisema kwa sasa mradi huo unafadhiliwa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph ambacho kimekuwa kikigharamia ununuzi wa vifaa na kwamba mazungumzo ya kushirikisha watafiti na watu wengine bado yanaendelea.
Alisema mazunguzo hayo ni kwaajili ya kushirikisha watafiti wa vyuo na taasisi za kitafiti za kigeni kusaidia kutoa utaalamu na mafunzo zaidi ya kiufundi, vifaa vya Satellite na huduma ya kuirusha Satellite hiyo angani.
Steven Makunga ambaye ni mmoja wa wavumbuzi wa Satellite hiyo, alisema wamefikia asilimia 50 ya kazi ya kuunda satellite hiyo na kwamba kwasasa tayari inaweza kutumika kukusanya baadhi ya taarifa.
Alisema chombo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwenye kupata taarifa za hali ya hewa na kwenye mawasiliano katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.
Makunga alisema itasiadia pia kutoa taarifa za kilimo kwa wakulima kuhusu mazao ya kupanda na maendeleo ya mazao yao kwa ujumla.
“Satellite hii pia inaweza kutusaidia katika elimu kwa kutoa maudhui ya elimu yetu Tanzania katika vijiji na maeneo ambayo hakuna miundombinu ya mtandao na huduma za simu na pia inaweza kurahisisha mawasiliano kwenye sekya ya afya,” alisema Makunga
Alisema inaweza pia kuwa msaada mkubwa yanapotokea majanga makubwa kama moto na mafuriko kwa kutoa taarifa za adharura kwa watu wanaokwenda kwenye maeneo ya uokoaji.