The House of Favourite Newspapers

Wanajamii Waaswa Kutokomeza Ukeketaji

0
Afisa Rasilimali Watu (HR) wa TGNP (aliyesimama) akitoa somo kwenye semina hiyo.

WADAU mbalimbali wametoa mchango wao namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwenye suala zima la ukeketaji na madhara yapatikanayo katika swala zima la ukeketaji wakati wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS) ikiwa ni semina ya kwanza ya mwaka 2021. Akizungumza kwenye Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazoandaliwa na (TGNP), Ofisa Program Idara ya Habari na Mawasiliano, Jackson Malangalila amesema kuwa, wanajamii wameeleza  namna ambavyo ukeketaji ulivyoleta madhara kwa jamii.

Washirikii wa semina hiyo wakisikiliza kwa makini yanayozungumzwa.

“Leo (Jumatano iliyopita) ni semina ya kwanza wa mwaka tumeona tuzungumzie na kujadili swala zima la ukeketaji ili kujua jamii inafahamu vipi na nini kifanyike ili kuweza kupinga ukatili huo na tumewasikia wadau walivyoeleza na kuonyesha uelewa wao na kitu gani kifanyike ili kuweza kuisaidia jamii inayokumbwa na ukeketaji.

“Tumewasikia wadau wakieleza madhara yanayopatikana kipindi cha mwanamke anavyofanyiwa tohara ikiwa ni kupata maumivu na kutokwa na damu nyingi wakati wa kukeketwa hivyo hupelekea kupoteza maisha, wakati wa kujifungua hutoka damu nyingi sana baada ya kovu kuachia kama tulivyomsikia mdau mmoja akitoa ushuhuda kwamba ndugu yake  ambaye amefanyiwa kitendo hicho alitoka damu nyingi na kuongezewa chupa sita za damu.

“Kuna mdau mwingine ametoa sababu ya wanawake kukeketwa ni mfumo dume kwamba kuna wanaume wengine wanapenda wanawake waliokeketwa kwa sababu ana kuwa hana hamu na tendo la ndoa hata kama akisafiri akirudi anakuta mke wake hana mahusiano mengine kwa kuwa amekosa hamu ya tendo la ndoa na ametoa mfano wa kabila la Wamasai wanaume wakienda kuchunga wanakaa muda mrefu wakirudi wanamkuta wake zao wako salama.

Semina hiyo ikiendelea.

“Nini kifanyike sasa ili kuona ukatili wa kijinsia kupitia ukeketaji unakomeshwa pia wadau wamezungumza kwamba sheria iwekewe mkazo kwa yule mkeketaji akikamatwa afungwe na pia wale wanaokeketa mara nyingi wamekuwa wakisema ndio kazi inayowaingizia kipato hivyo basi wameomba serikali na wadau wapewe njia mbadala ili wasitegemee ukeketaji.

“Pia Elimu itolewe mashuleni iwepo miongoni mwa mitaala ili watoto aweze kujifunza na kujua madhara ya ukeketaji kama wanavyofundishwa kuhusu (HIV), na pia kuna haja ya kuwashirikisha viongozi wa kimila kwa kuwa sasa hivi tamaduni zimebadilika.

“Aidha mdau mwingine amechangia kwa kusema  serikali iwezeshe maeneo mengi kupatikana maji kwa sababu kuna maeneo mengine hayana maji mtoto akipata muwasho sehemu za siri akimwambia mama yake anamwambia ana ugonjwa wa lawalawa hivyo mtoto hupelekea kuketetwa kumbe maji yangekuwepo mtoto mtoto asingewashwa angekuwa anatumia maji kujisafisha huenda ukawa na uchafu ndio humsababishia kuwashwa.” Alimaliza kusema Jackson.

Leave A Reply