The House of Favourite Newspapers

Wananchi Wafichua Manyanyaso ya Watumishi Kituo cha Afya Mwangika – Video

0


WANANCHI wa Kijiji cha Mwangika, Kata ya Bangwe, Jimbo la Buchosa, Mwanza, wamewalalamikia watumishi wa Kituo cha Afya Mwangika kwa vitendo vyao viovu vya kuwanyanyasa wagonjwa kwa kuwatukana, kuwatoza pesa bila kuwapa risiti, kuwauzia dawa binafsi wakati dawa zinazoletwa na Serikali hospitalini hapo zikiwa hazijulikani zinakopelekwa.

 

Wananchi hao wametoa malalamiko yao wakati wa mkutano wa hadhara na Mbunge wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo huku wakimtaka akifikishe kilio chao serikalini ili waweze kupatiwa huduma bora na stahiki.

 

“Mheshimiwa Mbunge, kero yetu sisi akina mama wajawazito tunapoenda pale Hospitali ya Mwangika kuanza kliniki tunatozwa Tsh 5,000, inaenda wapi? Bila hivyo hahudumiwi, je, hayo ndiyo maelekezo ya serikali kuwahudumia wajawazito? Kwa kweli tunateseka na tunanyanyasika, tusaidie,” alisema Mama Pili Stephano.

 

“Mimi nilikwenda pale kutibiwa, nilikuwa hatua za mwisho, daktari akasema bila kutoa tsh 300,000 sitafanyiwa oparesheni, kwa kweli isingepatikana hiyo laki tatu huenda sasa hivi ningekuwa marehemu. Juzi nimepeleka mwinga wangu kujifungua, kidogo ajifungulie mikononi mwangu, hii hospitali imekuwa jipu,” amesema Mzee Steven.

 

“Pale maabara kuna nesi mmoja ametawala sana ile hospitali, sisi tunashindwa kujua kwamba ile hospitali ni ya serikali au ya mtu binafsi? Kwa nini mtu mmoja atawale hiki kijiji? Mgonjwa yeyote awe mzee ni kutukanwa, mjamzito ni kutukanwa, kuna nini?” alisema  Josephan Mayunga.

 

Akijibu kero hizo, Mhe. Shigongo amesema hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali zenye huduma mbaya zaidi nchini kwani hata yeye ameshuhudia kwa macho yake.

 

“Mimi mwenyewe nimefika pale mara mbili, nimeshuhudia kwa macho yangu, hali niliyoiona pale ilinitoa machozi. Sasa mimi ninasema hospitali ile itabadilika. Tunamwambia Waziri wa Afya, dada yangu Mhe. Gwajima ajue kwamba hospitali hii ina huduma mbovu kwa wananchi wetu.

 

“Wananchi wanasema huduma mbaya, hakuna dawa, watumishi wana kauli mbaya, Mhe. Waziri ninakuomba utume timu yako ya wachunguzi pale, usipofanya hivyo mimi nitawashughulikia mwenyewe kabla wewe hujafika.

 

“Nimesikia kuna mama mmoja anafanya kazi maabara, eti ukipimwa maabara ukiandikiwa dawa ana dawa zake palepale, kwa nini huyu mtu anatutawala? Nimeshamuonya aache, akiendelea asinilaumu,” amesema Shigongo.

 

 

Leave A Reply