The House of Favourite Newspapers

Wanandoa Wenye Ajira Wanavyoweza ‘Kuwekeana Breki’ Za Kimafanikio!

HABARI za leo msomaji wangu, natumaini kuwa nguvu za Mungu zinakulinda na kukupatia ushindi katika matatizo ya maisha unayokutana nayo. Mpenzi msomaji, maisha ya sasa ni magumu tofauti na ya zamani, lakini kwa imani na umoja tunaweza kuyakabili. Wiki hii nakuja na jipya, nadhani macho yako yameona kichwa cha somo letu, hivyo nina imani kuwa utafuatana nami katika makala haya.

 

Mada ya leo ni nzito, inahitaji muda na ufahamu wa kutosha kuielewa na kuiweka katika vitendo. Nasema hivyo kwa kuwa inaingilia mazoea, tamaduni na baadhi ya imani.

Hivyo kuwaleta wasomaji pamoja itakuwa kazi ngumu, lakini ukweli nitakaouandika utasimama kuwa msaada kwa wanandoa na wapenzi ambao wana kipato.

 

Imezoeleka ndani ya jamii nyingi kuwa, mwenye jukumu la kutunza familia ni mume, kwamba huyu ndiye anayepaswa kutoa pesa kwa ajili ya matumizi ya ndani. Hilo halina ubishi, lakini tafakari, inakuwaje pale unapowafikiria wanandoa ambao wana kipato sawa, yaani mume anapokea mshahara na mke ni mfanyabiashara! Je, ni haki kwa mwanaume kuendelea kuwa mtoaji ndani ya familia? Ikiwa ndivyo, pesa za mwanamke zitakuwa na kazi gani?

 

Kimsingi, dhana ya mwanaume kuwa kiongozi wa familia na mtoa huduma inatumika vibaya, kwani husababisha upotevu mkubwa wa pesa, hasa zile zinazomilikiwa na wanawake, ambao hujiona kuwa hawana jukumu la kutunza familia.

 

Kama nilivyosema, desturi hii inaponza, kwani maendeleo ya wanandoa wenye kipato huwa madogo ukilinganisha na pesa wanazokusanya kwa mwezi au mwaka.

 

Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa, wanandoa wengi ambao wana kipato hawana maendeleo yanayokusudiwa, hii inasababishwa na wao kuachia mwanya wa kuwepo na pesa zisizokuwa na kazi.

Mara nyingi wanawake wamekuwa wakinyonya pato la wanaume kwa kisingizio kuwa wao ndiyo wanaopaswa kuhudumiwa kwa kila kitu.

 

Hata hivyo, lipo tatizo pia kwa baadhi ya wanaume, ambao wamekuwa na tabia ya kutumia mabavu kuchukua mishahara ya wake zao na kudai kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kupanga matumizi ya familia. Hilo nalo ni kosa kwani kumiliki pesa nyingi zikiwemo zile ambazo hukuzitolea jasho husababisha ongezeko la pato linaloshawishi matumizi holela.

 

Lakini, kuna jambo lingine ndani ya hili la kumiliki pesa zisizokuwa na kazi ndani ya familia. Wanawake wengi kwa mfano wamekuwa wakituhumiwa kuendesha mambo yao kwa siri kwa kununua viwanja, kujenga nyumba zao binafsi huku wakiendelea kuwa na hisa ndani ya mali za waume zao. Hii pia ni tabia mbaya ambayo imeziingiza ndoa nyingi katika migogoro mikubwa.

 

Hivi ni kweli kwamba wanawake hawana jukumu la kuhudumia familia kwa kununua chakula, mavazi na kugharamia malazi? Kama wanalo, ni utaratibu upi utumike kwa wanandoa ambao wana vipato toka vyanzo mbalimbali.

 

Je, mwanamke aachwe amiliki pesa zake bila kuingiliwa au mwanaume ana haki ya kufanya vyovyote atakavyo kwa kuwa yeye ni kichwa cha familia? Jibu ni hapana, nidhamu na mwongozo lazima uzingatiwe kama wanandoa wa jinsi hii wanataka maendeleo na uimara wa uhusiano wao.

 

Kwanza, kipato chochote kinachoingia ndani ya familia kiwe kinatoka kwa mume au mke, lazima kipangiwe malengo na wanandoa. Ikiwa ni mshahara, lazima uletwe pamoja ujadiliwe na uelekezwe wapi pa kwenda.

 

Kwa mfano kama mume anapokea 200,000 na mke 100,000, basi jambo la kwanza la kufanya ni kukutana kama kamati na kujadili nini cha kufanya kwa mwezi huo. Kama ni akiba shilingi ngapi zitakwenda benki, ngapi zitatumikia familia na ngapi zitasimamia matumizi ya dharura.

 

Aidha, baada ya makubaliano hayo suala la msingi litakalofuata ni kukubaliana juu ya nani mwenye haki ya kutumia pesa zaidi ya mwingine.

Kwa mfano, katika hali ya kawaida mke ana haki ya kupewa bajeti kubwa ya matumizi kwa mwezi kwa kuwa yeye ndiye anayebeba mzigo mkubwa ndani ya familia na kwamba mahitaji yake ya usafi na urembo ni ya juu kuliko mwanaume. Pia mwanaume ana harakati nyingi za kutafuta ziada kuliko mwanamke.

 

Pili, ieleweke kwamba, kila mwanaume/ mwanamke mwenye kipato ana jukumu la kutunza familia. Kile anachopata lazima kitumike kwa ajili ya wote. Zingatia hili lipo hata ndani ya kiapo cha ndoa kwamba hamtakuwa wawili, bali wawili katika umoja.

 

Siyo kweli kwamba mwanaume ndiyo wanaowajibika kwa asilimia mia moja kutunza familia. Kama haya niliyoandika yakizingatiwa na wanandoa wenye vipato sina shaka maendeleo yatapatikana kwao kwa muda mfupi sana.

Makala na Amran Kaima +255 658 798 787

Comments are closed.