The House of Favourite Newspapers

Wanaodaiwa Kumteka Mwandishi Waanikwa, Wahenyeshwa

NYUMA ya tukio la utekaji na udhalilishwaji wa mwandishi wa habari wa kujitegemea jijini hapa, Lucas Myovera, kuna kesi mbaya kufuatia kuanikwa kwa watu wanaodaiwa kuhusika na uhalifu huo, Uwazi limedokezwa.

Hivi karibuni Myovera aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana ambapo alipelekwa sehemu ya mtoni kisha kudhalilishwa na kurekodiwa akiwa mtupu kwa madai kwamba alifumaniwa na mke wa mtu hivyo kuibua taharuki nzito jijini hapa.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi jijini hapa liliingia mzigoni ambapo hadi sasa linawashikilia na kuwahenyesha kwa mahojiano watuhumiwa wawili.Miongoni mwa waliotiwa mbaroni ni mrembo ambaye anadaiwa kuwa ndiye chanzo cha tukio hilo anayefanya kazi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Mrembo huyo aliyetambulika kwa jina la Amina Mshana au Loveness inasemekana anafanya kazi kitengo cha masijala katika ofisi hiyo nyeti.Loveness alidaiwa kumrubuni Myovera kwa madai ya kutaka amwandikie habari zake.

Ilielezwa kuwa, Loveness na mtuhumiwa wa pili aliyetajwa kwa jina la Swalehe Mwindadi ambaye pia naye anafanya kazi kwenye ofisi hiyo ya Gambo kama Ofisa wa Protokali, Alhamisi iliyopita waliachiwa kwa dhamana.Hata hivyo, Ijumaa iliyopita ya Mei 18, mwaka huu, watuhumiwa hao walikamatwa tena na kwenda kufanyiwa upekuzi majumbani kwao.

Akizungumzia tukio hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Yusuf Ilembo alisema kuwa, watuhumiwa hao wanashikiliwa na Polisi na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Habari zilizopatikana kutoka kwa vyanzo mbalimbali vya Uwazi jijini hapa zilieleza kwamba, siku ya tukio, watuhumiwa hao waliendesha gari dogo aina ya Toyota IST, lililotumika kumteka mwandishi huyo na kumpeleka kusikojulikana akiwa amefungwa kamba, miguuni na mikononi.

TUJIKUMBUSHE SIMULIZI YA MYOVERA

“Siku ya tukio, Amina au Loveness kama alivyojitambulisha kwangu, alinipigia simu akidai ana mazungumzo na mimi, anataka anipatie habari yake ili niitoe kwenye chombo cha habari.

“Aliniambia habari yake inahusu mgogoro wake na mpenziye, Swalehe Mwindadi ambao wote wanafanya kazi ofisi moja.“Nilitoka nyumbani kwangu eneo la Mandela (Arusha Mjini), majira ya saa tatu usiku na aliniambia nimkute eneo la Ngulelo, umbali wa kilometa moja na nusu kutoka mjini.

“Baada ya kufika eneo hilo, nilimkuta akiwa kwenye gari ambalo baadaye nililitambua ni la Mwindadi ambaye alinitaka niingie ndani ili tuende eneo la Sakina kwa ajili ya maongezi.

“Hata hivyo, baada ya kuingia ndani ya gari, ghafla walikuja watu watatu waliokuwa wameficha nyuso zao kwa kitambaa cheusi na kunikaba wakiongozwa na Swalehe Mwindadi aliyenifunga kamba na kunipeleka kusikojulikana,” alidai Myovera na kuendelea:“Baada ya kutembea umbali fulani tukiwa kwenye gari, tulifika katika eneo ambalo silijui ambapo walinisukumia pembeni ya mto.

“Baadaye walinivua nguo zote na kuanza kunipiga mateke, ngumi na makofi huku wakinimwagia maji ya baridi yaliyokuwa yakitiririka mtoni na kuniambia kwamba wananitesa ili iwe fundisho kwa wanahabari wenzangu.“Kipigo na mateso vilikuwa kati ya saa tatu hadi saba usiku na walipotosheka, Mwandida aliwasiliana na polisi ambaye sikumfahamu.“Baadaye walinipeleka katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Ngarenaro.

“Tulipofika kituoni hapo walikuta kimefungwa na kuamua kunihamishia Kituo cha Polisi cha Kati.“Pale Kituo cha Polisi cha Kati walinifungulia kesi kuwa wamenikuta nikijaribu kuiba gari lao.

“Kituoni hapo polisi walitilia shaka maelezo hayo na kuamua kuwanyang’anya simu baada ya mimi kulalamika nilivyofanyiwa ndipo polisi wakakuta picha za video na za kawaida walizonirekodi wakati wakinitesa.

“Hapo ndipo polisi walipoamua kuwaweka chini ya ulinzi Amina na Mwandida kisha waliniandikia hati ya matibabu kwa ajili ya kwenda kutibiwa katika Hospital ya Rufaa ya Mount Meru ambako nililazwa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.“Lakini yote kwa yote ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru na ninaamini sheria itachukua mkondo wake.”

 

STORI: JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

Comments are closed.