The House of Favourite Newspapers

Wanaohangaika Kutafuta Ajira, ni Vyema Wakayajua Haya!

0

Amran Kaima| RISASI MCHANGANYIKO

NAOMBA nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mengi ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ipitayo ya maisha yangu.

Hakika amekuwa akinitendea miujiza mingi hali inayonifanya niamini kwamba, bila yeye hakuna ambalo ningeweza kulifanya na likafanikiwa. Kwa hilo nina kila sababu ya kumshukuru.

Ndugu zangu, wiki hii naomba nizungumzie jinsi ya kukabiliana na tatizo la ajira ambalo limekuwa likiwasumbua watu wengi kiasi cha kuwafanya baadhi yao kuathirika kisaikolojia na hata kufikia hatua ya kukata tamaa ya maisha.

Vijana wengi sana sasa wanasaka ajira bila mafanikio. Kila siku makundi mapya ya vijana waliomaliza elimu vyuoni yanaibuka na kupita sehemu mbalimbali kutafuta kazi za kuwawezesha kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Baadhi wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi na manyanyaso ambayo yamewaathiri kisaikolojia na kujikuta wakijiingiza katika kazi zisizokuwa halali na hatimaye kuyahatarisha maisha yao.

Kimsingi utafutaji wa kazi si suala rahisi kama baadhi wanavyofikiria hasa kwa Bongo ambapo ajira ni ngumu kiasi cha kuwafanya vijana wengi kuona ni rahisi kusoma kuliko kupata ajira.

Kutokana na hilo, wiki hii nimeona nikupe dondoo kadhaa ambazo ni vyema ukazijua ili kukabiliana na tatizo hili.

KUWA TAYARI KWA LOLOTE

Watafuta kazi wengi huwa hawako tayari kukabiliana na matokeo hasi. Mara nyingi wanapojaribu na kukosa hujiona kama ni watu wenye mikosi. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba, kuthubutu ndiyo mwanzo wa ushindi wa kila jambo.

Kwa maana hiyo unapoomba kazi kuwa tayari kupata jibu la umeshindwa. Hakuna ubaya pale mtu anapokosa baada ya kujaribu, kwani kushinda ni zao la majaribio.

Jiangalie wewe kama wewe

Watu wengi wamejikuta wakiathirika kisaikolojia kutokana na tabia ya kujilinganisha na wengine. Siku zote unapotafuta ajira simama kama wewe hata kama umemkuta rafiki yako aliyekuwa mbumbumbu darasani akiwa bosi katika kampuni fulani, usiangalie nyuma! Weka mbele bahati yako na usiilalie mlango wazi ya mwenzako.

NENDA TARATIBU

Wengi wanaotafuta ajira huwa na kasoro ya kufanya mambo kwa pupa, hujikuta wakitumia nguvu nyingi kwa wakati mmoja na kukimbia huku na huko kutwa nzima kutafuta kazi.

Mara nyingi watu wa aina hii huwa kama wendawazimu wakipita hata kwenye maofisi ambayo hayaajiri watu wenye taaluma zao.

Jambo hili ni baya kwani huwaondolea umakini na linachosha kwa kiasi kikubwa. Kinachotakiwa ni utulivu na ufuataji wa taratibu zilizopo za kutafuta kazi. Kwa mfano, mbali na matangazo ya kazi kutolewa kuwaruhusu watu wenye sifa kuandika barua za maombi, nchini kwetu kuna njia ya kutumia marefa ambao wamo ndani au karibu na waajiri. Njia hizi ni bora kuzitumia na zina heshima pia.

Wataalam wa masuala ya kisaikolojia wanaeleza kuwa, watu wengi wanaofanya mambo yao kwa pupa hukabiliwa na hatari kubwa ya kukata tamaa hasa wanapokutana na mikwamo ya hapa na pale.

Ni rahisi kwa mwenye pupa kukosa njia mbadala ya kupambana na kikwazo kutokana na ukweli kwamba wakati akishindana katika hatua za awali alitumia kiwango kikubwa cha nguvu, hivyo anapotafakari juhudi za kuongeza hujikuta akipata jibu la haiwezekani kushinda hata pale ambapo anaweza kushinda.

KAZI ZA KUJITOLEA

Ni vyema ukawa tayari kufanya kazi za muda ‘tempo’ au za kujitolea kuliko kukubali kukaa nyumbani huku ukisubiri ajira ya muda mrefu. Tambua kwamba, unapokuwepo kazini aidha kwa kujitolea, kwa muda mfupi au kwa mshahara kidogo kunakuwezesha wewe kupata uzoefu wa kazi lakini pia kufahamika kiasi cha kukufanya ujiweke katika nafasi nzuri ya kupata ajira nzuri.

MSIMAMO NI MUHIMU

Wasomi wengi wamejikuta wakipoteza mwelekeo wa maisha yao kwa kukubali kufuata upepo wa ajira unavyotaka. Kwa mfano unaweza kumkuta mwandishi baada ya kukosa kazi ya uandishi akajiingiza katika biashara. Kibaya zaidi atakuwa mfanyabiashara bila kuwa na malengo ya kurudia mstari wake wa uandishi.

Inashauriwa kila mmoja kufuata kile alichosomea na endapo atabadili iwe ni kwa mwelekeo wa muda au ule aliouchagua na isiwe tu kwa sababu amekosa ajira.

Kwa leo naomba niishie hapo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

KWA MAONI: +255 658 798787

Leave A Reply