The House of Favourite Newspapers

Wanaojuta Leo, Kuna Sehemu Walikosea, Amua Sahihi Sasa!

NA Amran Kaim | RISASI JUMATANO| UTAJIRI

Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii inayoyagusa maisha yetu ya kila siku nikiamini kwamba, Mungu amekubariki na unaendelea vyema na mishemishe zako za kila siku.

Mimi namshukuru Mungu kwani amekuwa akinijaalia kila la heri na kuniepusha na yale ya shari katika maisha yangu. Kwa hilo niseme tu kwamba, Asante Mungu!

Pia niseme asante Mungu kwa kunipa uwezo wa kuandika mada mbalimbali ambazo zimekuwa  msaada mkubwa kwa jamii inayonizunguka. Na nikuhakikishie tu kwamba, kama utaendelea kuwa mfuatiliaji wa kile ninachoandika, lazima maisha yako yatabadilika.

Mpenzi msomaji wangu, leo nataka kuzungumzia umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ambayo yatatufanya tupate kile tulichokitarajia hasa kutokana na ukweli kwamba, dunia yetu ina vitu vingi ambavyo vinatulazimisha kuwa makini katika kuchagua ili tupate vilivyo bora.

Duniani kuna wanawake wengi wazuri, lakini si wote wanaofaa kuoa, wanaume wapo wengi, kazi ziko nyingi, elimu, vitu, mavazi, vyakula, dawa na shule. Kila unaloweza kuwaza linapatikana kwa wingi.

Hivyo ni jukumu la mwanadamu mwenyewe kufanya maamuzi sahihi ili aweze kufikia kilele cha ubora anaouhitaji katika maisha yake. Hii ni kwa sababu, maamuzi yaliyo sahihi ndiyo yanayoweza kukupatia majibu sahihi na maamuzi ya kukurupuka siku zote mwisho wake ni kujuta.

Ikiwa mwanamke alikuwa ukiota kuwa na mume mpole, mwenye kumheshimu na kumpenda kwa dhati na akajikuta amempata aliye tofauti, ajue kwamba alifanya maamuzi mabaya ya kuwa na uhusiano na mwanaume huyo. Huu ndiyo ukweli kwamba watu wengi wameshindwa kuchagua mazuri na sasa wanalia na mabaya waliyoyachagua wenyewe.

Kadhalika, juhudi wanazotumia wanaume waliooa wanawake wasiojua nini maana ya ndoa ni kubwa zaidi ukilinganisha na zile ambazo wangetumia kuchagua wanawake wema wa kuwafaa maishani mwao.

Ndiyo maana mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kuwa, mtu mwenye busara lazima aitumie kabla ya kufanya maamuzi na siyo baada ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi.

Wachache sana hutumia busara wanapochagua, wengi wao wanapopata matokeo mabaya ndipo huanza kutumia busara kuyakabili wakati walikuwa na nafasi ya kufanya hivyo kabla na wakaona mafaniko sahihi.

Tunapobahatika kupata pesa nyingi kwa mfano, tunakuwa na mipango ishirini au zaidi. Mara kununua gari la biashara, mara kufungua duka, hoteli na hata kulima, lakini tunazembea katika kuchagua na kujikuta tumeangukia kwenye uchaguzi mbaya ambao mwishowe hutuhuzunisha.

Niseme tu kwamba ili tuweze kuwa na maisha mazuri tuna kila sababu ya kuwa makini sana katika kuamua na kuwa na uhakika kwamba mwisho wa maamuzi tunayoyafanya leo ni kupata kile tulichokitarajia.

Tunaweza kufikia maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi wetu kwa kuzingatia yafuatayo. Kwanza ni kutambua mahitaji yetu na kuyaorodhesha kwa lengo la kupata dira ya kuelekea kwenye uchaguzi mzuri.

Pili, kwa kuwa dunia ina vitu vingi vya kufanana sawa na unavyohitaji ni vema ukatulia katika mawazo kwa muda mrefu kabla ya kufikia maamuzi. Tafakari kwa kulinganisha vitu unavyoviona na malengo yako kisha hakiki majibu unayopata kwa kila hatua.

Kumbuka tu kwamba, wengi unaowaona leo wanajuta kwa kutopata yale waliyoyatarajia, walikosea kwenye kuamua, hivyo kufanya maamuzi sahihi leo ni kuepuka kuja kujuta kesho na keshokutwa.

Kwa leo niishie hapo, kama una lolote ambalo linakutatiza na ungependa kupata ushauri kutoka kwangu, usisite kuwasiliana na mimi kupitia namba zilizopo hapo juu.

Comments are closed.