The House of Favourite Newspapers

Wanawake WCF Watoa Msaada Gereza la Segerea

0

Wafanyakazi wanawake wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wanawake mahabusu na wanaotumikia kifungo katika Gereza la Segerea Jijini Dar es Salaam ikiwa sehemu ya kurejesha kwa jamii katika kuelekea siku ya wanawake duniani, 2024.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF Bi. Laura Kunenge, amesema kwa kutambua majukumu makubwa anayobeba mwanamke kwenye jamii, wanawake wa WCF wameona ni vema kuwashika mkono wanawake wenzao ambao wana uhitaji.
“Tunafahamu kwamba serikali inafanya jitihada kubwa katika kuwahudumia wafungwa na mahabusu lakini na sisi tumeona katika kuadhimisha siku yetu tuwashike mkono wenzetu, WCF tunajua ukimsaidia mama umesaidia jamii nzima, na wenzetu waliopo hapa wakitoka watakuwa wamejifunza na watasaidia jamii zao, amesema Bi. Laura.


Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Wanawake, Gereza la Mahabusu Segerea, SP. Hamida Mussa Matimba ameshukuru wanawake wa WCF kwa kuona umuhimu wa kuwakumbuka wanawake wenzao, na amesema kuwa msaada huo wa mahitaji muhimu utawasaidia sana wanawake hao, na hasa wale ambao wana watoto wadogo.
Katika hatua nyingine, Wanawake wa WCF waliungana na wanawake wafanyakazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwa ni Mfuko wa pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutoa msaada wa vifaa tiba , mahitaji muhimu na kulipia gharama za matibabu kwa baadhi ya watoto wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika wodi ya watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Siku ya Wanawake duniani huadhimishwa Machi 8, kila mwaka ambapo mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo wekeza kwa mwanamke kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.

Leave A Reply